Na. Josephina Kayugwa, MIYUJI
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imechagua kimkakati eneo la ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Miyuji B ili kuweza kuwahudumia wananchi wengi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akitoa maelezo ya utangulizi kwa Kamati ya Siasa Mkoa wa Dodoma iliyotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Miyuji B iliyopo Kata ya Miyuji jijini Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisema kuwa eneo la ujenzi wa shule hiyo limechaguliwa kimkakati katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwa katikati ya maeneo ya wananchi na karibu na eneo zitakapojengwa nyumba 3,500 na Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA).
“Niwapongezi Diwani wa Kata ya Miyuji, Mheshimiwa Beatrice Ngerangera na Mkuu wa shule ya Miyuji, Mwl Greyson Maige kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa shule hii. Tulishauri pia kisima kuchimbwa katika eneo hili kwa lengo la kupata maji ya uhakika. Jukumu la wazazi sasa ni kuwapeleka shule watoto wao na kutafsi elimu watakayoipata kwenye fursa ya ajira” alisema Alhaj Shekimweri.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Miyuji B, Mkuu wa Shule ya Sekondari Miyuji, Greyson Maige alisema kuwa shule hiyo inakwenda kuwaondolea hadha wanafunzi ya kutembea umbali mrefu na kufika shuleni kwa wakati. Faida za mradi huu utakapokamilika ni kuwasaidia wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutembea umbali mfupi na kufika shule kwa wakati. “Faida nyingine ni kupunguza idadi ya wanafunzi Shule ya Sekondari Miyuji ilipo Kata ya Mnadani na kupunguza mimba za utotoni pamoja na utoro wa wanafunzi. Kwa upande wa walimu watakaa kwenye mazingira ya shule na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuwezesha mazingira mazuri ya kuishi kwa walimu” alisema Mwl. Maige.
Shule ya Sekondari Miyuji ilipokea kiasi cha fedha shilingi 544,225,626 tarehe 30 Juni, 2023 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya katika Kata ya Miyuji iliyopo eneo la Mpamaa kupitia mradi wa SEQUIP (Mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya elimu).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.