HALMASHAURI ya jiji la Dodoma imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 40 katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2018 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani, hivyo kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wake na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa Madiwani katika mkutano wa kawaida wa baraza la Madiwani kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2018/2019 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Katika mkutano huo, baadhi ya wajumbe walitaka kujua Jiji limekusanya mapato kiasi gani katika robo ya pili ya mwaka huo wa fedha.
“Katika kipindi cha kufikia robo hii ya pili, Halmashauri ya jiji la Dodoma imekusanya shilingi bilioni 40.16 sawa na asilimia 60 ya mapato ya ndani ya nusu mwaka. Mwezi Disemba, 2018 tulikusanya shilingi bilioni 16 kiasi ambacho ni zaidi ya baadhi ya Halmashauri nyingine kwa mwaka” alisema Kunambi na kusisitiza kuwa ukusanyaji huo ni wa kujivunia.
Akijibu hoja ya ukarabati wa ukumbi wa Halmashauri, Mkurugenzi huyo alisema kuwa kiasi cha shilingi Milioni 200 kilipitishwa na Baraza la Madiwani ili kuanza ukarabati wa ukumbi huo.
“Ukarabati wa ukumbi umekamilika kwa asilimia kubwa, ila bado tunahitaji visemea (microphones) ili baraza letu liwe la kisasa...tuna changamoto ya viti ambavyo mkandarasi ameviagiza kutoka nje ya nchi na tunategemea ifikapo Februari 15, 2019 ukumbi utakuwa umekamilika” alifafanua Kunambi.
Alisema Halmashauri inaendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji ya kodi mbalimbali hali inayosaidia kutekeleza miradi ya maendeleo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.