Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imekopesha shilingi 1,108,000,000 kwa vikundi 61 vya vijana katika utekelezaji wa mkakati wake wa uwezeshaji vijana kiuchumi kupitia asilimia nne za mikopo itokanayo na mapato ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mufungo Manyama alipokuwa akiwasilisha mada ya fursa za vijana katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kikao cha wadau wa afua za afya ya uzazi na maendeleo ya vijana kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo.
Manyama alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021, halmashauri ilitoa mikopo kwa vikundi 61 vya vijana yenye thamani ya shilingi 1,108,000,000. Alisema kuwa fedha hizo zilitolewa kugharamia miradi ya uwezeshaji vijana kiuchumi. “Miradi hiyo iligawanyika katika sekta za kilimo cha bustani za mbogamboga na matunda, ufugaji, ufundi, bodaboda, biashara ndogondogo. Sekta nyingine ni usindikaji wa vyakula, ujenzi, huduma za vyakula na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano” alisema Manyama.
Akiongelea utaratibu na sifa za kupata mikopo hiyo ya asilimia nne kwa vijana, alisema kuwa halmashauri inatoa mikopo hiyo yenye masharti nafuu kwa vijana waliojiunga katika vikundi vya watu watano na kuendelea. “Vikundi hivyo lazima viwe vimesajiliwa na vina vijana kuanzia umri wa miaka 15-35 na wawe na akaunti benki. Vikundi hivyo, lazima viwe na maandiko mafupi ya miradi yatakayoonesha mradi unaoombewa fedha na gharama zake” alisema Manyama kwa msisitizo.
Awali akitoa neno la utambulisho, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Asha Vuai alisema kuwa changamoto kuwa iliyopo ni kuwafanya vijana waweze kujitambua na kuwa wawajibikaji katika jamii. “Baadhi ya vijana siyo waaminifu hasa kwenye kufanya marejesho ya mikopo wanayokopa. Tofauti na akina mama, wengi ni waaminifu kwenye kufanya marejesho ya mikopo. Hata ukiangalia kwenye madeni, wengi wanaodaiwa ni vijana. Serikali ina lengo zuri la kuwawezesha vijana kiuchumi ndiyo sababu mikopo hiyo haina riba” alisema Vuai kwa masikitiko.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Asha Vuai (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baada ya kikao cha wadau wa afua za afya ya uzazi na maendeleo ya vijana kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.