Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetoa shukrani kwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya elimu ya awali na msingi kwa kuwahakikishia wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia.
Shukrani hizo zilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya awali na msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Myalla alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu chini ya mradi wa kuboresha upatikanaji wa fursa sawa katika ujifunzaji bora wa elimu ya awali na msingi Tanzania bara (BOOST) kwa shule ya msingi Chang’ombe na Swaswa katika Jiji la Dodoma.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya elimu ya awali na msingi kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Miundombinu hii imekuwa chachu ya maendeleo ya elimu na taaluma. Leo nimetembelea kukagua maendeleo ya ujenzi katika shule ya msingi Chang’ombe. Ujenzi katika shule hiyo upo katika hatua nzuri. Wapo hatua ya kupaua na tayari wameshapiga bati kwa baadhi ya maeneo ya madarasa. Na huko nimewasisitiza kuongeza kasi ili kukamilisha ujenzi kwa wakati.
Hapa Kata ya Ipagala inajengwa shule ya msingi Swaswa ambayo ni mpya kabisa. Kama tunavyoona ujenzi unaendelea ukiwa hatua ya lenta na mafundi wapo eneo la mradi. Nimewasisitiza kuongeza kasi ya ujenzi ili ifikapo tarehe 10 Juni, 2023 kazi iwe imekamilika” alisema Myalla.
Kwa upande wa Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Ipalaba B, Praxeda Fundisha alisema kuwa shule yake ilipokea shilingi 318,800,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa tisa, jengo la utawala na matundu 16 ya vyoo. “Kama mnavyojionea leo ni wikendi lakini mafundi wanaendelea na kazi wakifunga lenta na wengine wanafunga mbao za kenchi. Ujenzi wa shule hii utafanya kazi ya ufundishaji kwa walimu kuwa rahisi kwa sababu watoto watakuwa wamepungua darasani. Mfano shule ya Ipagala B, mkondo mmoja unafika wanafunzi 120 kwa darasa moja. Hivyo, kupungua kutakuwa kumewarahisishia sana walimu na wanafunzi ufaulu utapanda” alisema Fundisha.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Swaswa, Charles Nyuma alisema kuwa mtaa wake una wananchi wengi katika Kata ya Ipagala kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi iliyopita. “Tuna takribani wananchi 10,941. Mtaa wetu ulikuwa hauna shule ya msingi. Mtaa kilio chetu ilikuwa ni kupata shule ya msingi. Watoto wetu wanatembea umbali mrefu kwenda shule wakivuka mapori na makorongo jambo ambalo ni hatari kwao. Kwa kweli serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan hakika tunaishukuru sana jinsi ilivyotupatia shule hii” alisema Nyuma.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa shule ya msingi Swaswa, Samwel Bosco alimtaja Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ameikumbuka sana sekta ya elimu. “Elimu ndiyo kila kitu kwa Maisha ya sasa na vizazi vijavyo. Tunategemea shule hii mwezi Julai, 2023 ianze. Tupo saiti tunafanya kazi usiku na mchana na tutahakikisha pesa inatumika ipasavyo bila hata msumali kupotea bali kutumika pale unapotakiwa kutumika” alisema Bosco.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipokea shilingi 1,654,000,000 kutoka mradi wa BOOST kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi ikiwa ni ujenzi wa shule nne mpya na ujenzi wa madarasa kadhaa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.