Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, ametembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuelezwa shughuli zinazotolewa katika banda hilo kwa upande wa Divisheni ya Kilimo Mjini.
Alielezwa kuwa Kilimo Mjini kinahusiana na kilimo cha kisasa kinachojikita katika mbogamboga na matunda kutokana na ufinyu wa maeneo ya mjini wanapoishi wakulima.
Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Athumani Mpanda alieleza kuwa wakulima wanapaswa kutumia maeneo yao madogo waliyonayo kwaajili ya bustani kiroba. “Hizi bustani kiroba tunazitumia kupanda mbogamboga ambazo familia itatumia na hii ni kwasababu kama una kiroba cha kustawisha maua ambayo huyatumii ni vizuri kutumia kuotesha mboga mboga ambazo zitajumuisha lishe na kupendezesha mazingira yetu” alisema Mpanda.
Aliongeza kuwa elimu ya bustani za majumbani imeendelea kutolewa katika taasisi nyingi za serikali pamoja na shule za msingi na sekondari. “Tumeanzisha elimu hii kwa lengo la kuhakikisha wakulima na wale wapenzi wa mboga mboga wanapata lishe bora. Hadi sasa tumefikia asilimia 50 ya kaya zote za Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kuwapelekea elimu hii. Kila mwaka tuna mpango wa kutoa elimu ya lishe majumbani kupitia vikundi, taasisi na hata wakulima wa kaya moja moja. Lakini pia tuna programu maalum ya uendelezaji wa lishe kwenye jamii inayofanyika kila mwaka” aliongeza Mpanda.
Nae, Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga baada ya kusikiliza maelezo hayo alisema kuwa sekta ya kilimo inapaswa kuwekewa mkakati madhubuti wa kuhakikisha mazao yanayolimwa yanatoa lishe bora kwa walaji.
Aliongeza kuwa umakini unahitajika katika usimamizi wa sekta ya kilimo. “Kilimo mjini ndio habari ya mjini kwasasa, sekta hii inahitaji kuangalia kwa karibu kilimo hiki kilichogeuka biashara, wapo watu hawazingatii utaratibu wa namna ya kulima na badala yake wanalima katika mazingira machafu ambayo yanapelekea mbogamboga na matunda kukuwa katika uchafu na kubeba vimelea vya maradhi. Kwa maana hiyo muangalie hilo na kuhakikisha mnawakagua na kutoa elimu ya kutosha” aliongeza Dkt. Mganga.
Banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma pamoja na seksheni za kilimo, mifugo na uvuvi zinatoa huduma mbalimbali ikiwemo elimu ya teknlojia ya kilimo, ufugaji na uvuvi, uuzaji wa viwanja vya matumizi mbalimbali, elimu ya mikopo ya asilimia 10, elimu ya lishe bora, elimu ya unyonyeshaji maziwa ya mama, elimu ya umuhimu wa Leseni ya Biashara na ukataji wa leseni ya Biashara na fursa za uwekezaji zilizopo katika Jiji la Dodoma.
MWISHO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.