HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetekeleza agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Selemani Jafo la kuzitaka Halmashauri zote nchini kuwa na vipando katika eneo la maonesho ya Nanenane kwa mwaka mzima ili wananchi wapate fursa ya kujifunza.
Kauli ya utekelezaji huo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika, Yustina Munishi alipokuwa akiongelea utekelezaji wa agizo hilo ofisini kwake jana.
Munishi alisema “mtakumbuka wakati akifunga maonesho ya Nanenane mwaka 2019/2020 katika viwanja vya maonesho vya Nanenane, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Selemani Jafo aliziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinakuwa na vipando mwaka mzima. Uwepo wa vipando hivyo utawawezesha wananchi kupata fursa pana zaidi ya kujifunza tofauti na kusubiri msimu wa maonesho ya Nanenane. Sisi tumetekeleza agizo hilo na kuweka katika mipango yetu. Utekelezaji wa agizo hilo pia ni utekelezaji wa Ilani ya chama kilichopo madarakani kwamba wananchi wawezeshwe kupata teknolojia bora za kilimo”.
Akiongelea uendelevu wa agizo hilo, alisema kuwa Halmashauri imechimba kisima kirefu katika eneo la maonesho ya Nanenane kwa lengo la kuwa na uhakika wa maji. Katika bajeti ya 2019/2020 shilingi milioni 40 ziliwezesha kuweka pampu na tenki la kuhifadhia maji na kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwa njia ya matone, aliongeza.
Halmashauri imefanikiwa kuwajengea uwezo wananchi katika matumizi ya teknolojia katika kilimo cha nyanya. “Tunaweza kuzalisha nyanya kwa njia ya kitalu nyumba, na tumetoa elimu hiyo kwa wananchi juu ya matumizi ya kitalu nyumba. Katika awamu ya kwanza jumla ya vijana 100 wamepewa mafunzo ya matumizi ya teknolojia ya kitalu nyumba. Tunaona hiyo ni njia pekee ya kuwafundisha vijana matumizi ya teknolojia ili kuleta tija katika kilimo na kupata fursa za kiuchumi kwa sababu unalima eneo dogo lakini unazalisha kwa tija kubwa” alisema Munishi.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika maonesho ya Nanenane ili kunufaika na elimu inayotolewa bure kuhusu kilimo, mifugo na uvuvi.
Maonesho ya Nanenane mwaka 2020 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kwa Maendeleo ya kilimo, Mifugo na Uvuvi, chagua viongozi bora 2020”.
Kwa upande wa kijana kutoka kikundi cha Maarifa John Samweli alisema kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kupata uelewa wa matumizi ya teknolojia ya kitalu nyumba katika kilimo cha nyanya, pilipili hoho na matango. “Mafunzo haya yatatusaidia kujitegemea hata nje ya kikundi hiki, tunaishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutupatia mafunzo ya mwezi mmoja na mkopo wa shilingi milioni saba (7,000,000).
Bustani ya Vitunguu maji.
Kitalu nyumba kwa kilimo cha ndani
Zao la mtama
Kabichi
Zao la Alizeti
Zao la bilinganya
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.