HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi 545,000,000 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2020/2021 ili kuviinua vikundi hivyo kiuchumi.
Hayo yalikuwa kwenye taarifa ya utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge, taarifa iliyosomwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mafuru katika halfa ya kukabidhi mikopo hiyo iliyofanyika katika bustani ya Nyerere ‘square’ jana.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetenga jumla ya shilingi 2,262,708,770 kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. “Katika robo ya kwanza Julai-Septemba, 2020, Halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 545,000,000. Vikundi saba vya wanawake vimepewa shilingi 125,000,000, vikundi viwili vya vijana vimepewa shilingi 378,000,000 na vikundi vitano vya watu wenye ulemavu shilingi 42,000,000. Vikundi hivyo vimekopeshwa ili kutekeleza miradi ya usafirishaji na kupewa bajaji na bodaboda, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ujenzi wa machinjia ya kuku, utengenezaji wa bidhaa za ngozi, saluni na ushonaji” alisema Mafuru.
Akioelezea historia ya mikopo hiyo, alisema kuwa Halmashauri ilianza kutoa mikopo kwa makundi maalum mwaka wa fedha 2015/2016. “Kuanzia mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2019/2020, mikopo iliyotolewa kwa makundi hayo ni shilingi 5,292,829,899. Vikundi 812 vya wanawake vimenufaika na shilingi 3,254,962,583, vikundi 425 vya vijana vimenufaika na shilingi 1,856,537,316 na vikundi 30 vya watu wenye ulemavu vimenufaika na shilingi 181,330,000” alisema mkurugenzi huyo.
Kuhusu ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo hiyo, aliutaja kuwa unaendelea vizuri. “Hadi kufikia mwezi Septemba, 2020 kati ya shilingi 5,292,829,899 zilizokopeshwa, shilingi 2,526,769,984 zimerejeshwa na kiasi kilichobaki ufuatiliaji unaendelea” alisema Mafuru.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa mikopo ya bodaboda 46, bajaji 20 na guta moja kwa vikundi vya vijana zenye thamani ya shilingi milioni 378 kati ya mikopo ya shilingi milioni 545 iliyopokesha makundi maalum robo ya kwanza Julai-Septemba, 2020.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.