Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepunguza utegemezi wa kibajeti katika chanzo cha mauzo ya viwanja kwa shilingi bilioni 11 ikijipanga kuboresha huduma kwa mwananchi analeyengwa moja kwa moja na bajeti hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe katika Mkutano wa Baraza la Madiwani maalum kwa ajili ya kujadili rasimu ya Mpango na Bajeti wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2024/2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Prof. Mwamfupe alisema “katika bajeti hii ni kupunguza utegemezi katika chanzo cha mauzo ya viwanja. Katika bajeti iliyopita tulikuwa na shilingi bilioni 29 tunazitegemea katika mauzo ya viwanja. Leo hii tumepunguza hadi shilingi bilioni 18. Napenda niwasisitizie wataalam wetu, mahitaji ya viwanja hayajapungua kwa kiasi kikubwa sana. Bado wananchi wanahitaji viwanja. Sekta ya ujenzi inazidi kushamiri kila asubuhi. Sehemu kubwa ambayo inadibi tuweke mkazo ni kuboresha huduma ili watu wavutike na viwanja tunavyouza sisi badala ya kwenda kwenye viwanja vingine ambavyo havina uhakika. Kama leo katika zoezi la kliniki tuliweza kutoa vibali vya ujenzi 4,470 kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, 2023 tunataka tuwe na kasi hiyohiyo tuliyoanza nayo tuendelee nayo. Sisi ndiyo wenye ardhi, jukumu la kupanga na kumilikisha ardhi ni letu”.
Mstahiki Meya alisema kuwa bajeti hiyo imemlenga mwananchi wa kawaida moja kwa moja. “Ndiyo maana tukaweka mkazo mkubwa katika sekta ya elimu na afya. Katika bajeti hii tumejikita zaidi kukamilisha miradi viporo ambavyo ni kipaumbele ili kuunga juhudi za wananchi katika maeneo ya pembezoni mwa halmashauri yetu. Bajeti ni ukusanyaji wa mapato na matumizi. Tusipokusanya hatuna cha kutumia, lakini sisi tunaamini kwa nguvu tuliyoanza nayo tunaamini sana wote tutafanikiwa. Mkurugenzi tungependa kusikia upimaji kazi wa watendaji kwa maafisa wako unajikita wameshiriki namna gani katika ukusanyaji mapato” alisema Prof. Mwamfupe.
Mwenyekiti huyo alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa miongozo yake kwa halmashauri. Vilevile, alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kwa jinsi anavyoishauri halmashauri na kusema uelewa wake kwa masuala ya halmashauri hauna kifani.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.