Na. Dennis Gondwe, CHIHANGA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inatambua jitihada zinazofanywa na mwanamke wa kijijini katika uzalishaji wa chakula na kusimamia lishe ya familia.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Charity Sichona alipokuwa akiongea maadhimisho ya siku ya mwanamke anayeishi kijijini ofisini kwake leo ambayo yatafanyika katika Kata ya Chihanga jijini Dodoma.
Sichona alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaadhimisha siku hiyo kwa lengo la kuendelea kutambua jitihada za mwanamke anayeishi kijijini. “Wanawake wanaoishi vijijini wanamchango mkubwa katika kuzalisha chakula na kuchangia uwepo wa chakula katika familia na nchi nzima. Hivyo, serikali imeamua kutambua jitihada zao za kilimo, ufugaji na shughuli za kiuchumi na kuwatia moyo ili waendelee kuzalisha wakati serikali ikiendelea kutatua changamoto zinawakabili” alisema Sichona.
Sichona alisema kuwa mwanamke wa kijijini anapowezeshwa kufanya shughuli zake bila vikwazo familia, halmashauri na taifa kwa ujumla litakuwa na uhakika wa chakula na hadi kuwa na chakula cha akiba. “Mwanamke ni mtendaji mzuri katika kazi za uzalishaji. Hii siku inatambua zile jitihada zinazofanywa na mwanamke huyu ili kuzipa thamani” aliongeza.
Akiongelea baadhi ya program zinazowezeshwa na serikali alisema kuwa zipo kwa ajili ya kuwasaidia wanawake kukua kiuchumi. “Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha program mbalimbali. Mfano Kizazi cha Usawa, hii inatambua jitihada za wanawake wanazofanya na wanapewa elimu juu ya uzalishaji, masuala ya kilimo, mifugo na kazi za mikono ili kuendeleza uchumi wao na kuleta usawa katika kumiliki mali na ardhi ili mwanamke awe na usawa katika masuala ya kiuchumi” alisema Sichona.
Kwan upande wake mkazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Hadija Sued alisema kuwa ni mara yake ya kwanza kusikia maadhimisho hayo. Alisema kuwa maadhimisho hayo ni muhimu kwa sababu yatawahamasisha wanawake kuongeza juhudi katika shughuli zao za uzalishaji mali.
Maadhimisho ya Siku ya mwanamke anayeishi kijijini mwaka 2023 yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Wezesha wanawake vijijini kwa uhakika wa chakula; lishe na uendelevu wa chakula”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.