MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge amesema kuwa ili Jiji la Dodoma liweze kuvutia kwa maendeleo lazima liwe na vitu muhimu pamoja na maisha bora kwa wananchi wake.
Mkuu wa Mkoa alisema hayo katika ziara yake ya kutembelea na kukagua mradi wa maji wa muda mfupi unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) wa uchimbaji visima eneo la Ihumwa ikiwa ni mpango wa muda mfupi wa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji jijini hapa.
Dkt. Mahenge aliyataja mambo muhimu yatakayoweza kuleta maendeleo kwa kasi katika Jiji hilo kuwa ni miundombinu safi ya usafirishaji, upatikanaji wa maji, afya na mazingira bora na rafiki katika elimu.
Mkuu huyo wa Mkoa aliishukuru Serikali Kuu kupitia Wizara ya Maji kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni moja na kuipatia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuchimba visima kwa muda mfupi ili kutatua kero za upatikanaji maji mjini Dodoma.
“Ili Jiji la Dodoma liweze kuvutia na ni utaratibu wa majiji yote duniani lazima yaweze kuwa na mambo muhimu ikiwemo maisha bora kwa wakazi wa maeneo husika. Hivyo, napenda kuishukulu Serikali Kuu kwa kuimarisha kwa kiasi kikubwa mambo hayo muhimu ambayo ni miundombinu ya usafirishaji, afya, maji, mazingira bora na rafiki ya elimu” alisema Dkt. Mahenge.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema kuwa kupitia Wizara ya Maji wametoa shilingi billioni moja kwa DUWASA kwa ajili ya kutekeleza mradi wa muda mfupi wa uchimbaji wa visima mjini hapa.
Aliongeza kuwa “Serikali kupitia Wizara ya Maji imeamua kuipatia DUWASA shilingi bilioni moja kwa ajili ya kutekeleza mradi huu wa kuchimba visima katika maeneo mbalimbali ikiwemo hapa Ihumwa. Kutokana na ongezeko la uhitaji wa Maji jijini Dodoma, tumeamua DUWASA watekeleze kwanza mradi huu wa muda mfupi ili kutatua kero za upatikanaji wa maji mjini hapa.
Sisi kama Wizara tunayo miradi ya muda mrefu, tunaendelea kuusanifu kwa kina mradi huo wa kuunganisha mtandao wa Maji kutoka Ziwa Victoria kuja mpaka hapa Dodoma“ alisisitiza Mhandisi Sanga.
Aidha, kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji (DUWASA), Mhandisi David Pallangyo alisema mradi huo wa muda mfupi wa kuchimba visima utatekelezwa katika maeneo kadhaa jijini hapa kwa kuzingatia ongezeko la uhitaji wa maji.
Hata hivyo, Mhandisi huyo ametoa tathimini ya kukamilika kwa mradi huo ambao utatumia muda wa miezi miwili mpaka mitatu kwa kuchimba visima vyenye urefu wa mita 150.
“Sisi kama DUWASA kufuatia kuongezeka kwa uhitaji wa Maji katika maeneo mbalimbali jijini Dodoma tumeona kuja na mradi wa muda mfupi ambao utapuguza changamoto za upatikanaji maji mjini.
Kwa utekelezaji wa kuchimba visima hivi sio kwa eneo hili moja la Ihumwa, bali tutachimba maeneo mbalimbali visima vyenye urefu wa mita 150 ambapo tutatumia muda wa miezi miwili mpaka mitatu“ alisema Mhandisi Pallangyo.
Kwa habari zaidi bofya hapa: DUWASA kutumia Bilioni 2.4 kuchimba visima Dodoma (HabariLeo)
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) akijadiliana na Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi David Pallangyo alipotembelea na kukagua mradi wa maji wa muda mfupi unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA).
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge (wa pili kulia) akijadiliana kitu na Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kushoto) wakati zoezi la uchimbaji kisima likiendelea Ihumwa alipotembelea mradi huo wa uchimbaji visima Jijini Dodoma unaoendelea.
Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi David Pallangyo akifafanua kuhusu Mradi wa Muda Mfupi wa Uchimbaji Visima mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani).
Mafundi wakiendelea na kazi ya kuchimba visima.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.