WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Innocent Bashungwa ameielekeza Mikoa yote nchini kupitia Wakuu wa Mikoa kubuni maeneo ya machinga na kujenga miradi ya kuwapanga kulingana na mazingira Mkoa husika yatakayowaezesha wateja wao kuwafikia.
Waziri Bashungwa ameelekeza hayo leo Machi 09, 2022 wakati alipoambatana na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kutembelea mradi wa ujenzi wa Soko la Wafanyabiashara Wadogo (Machinga Complex) lililoko barabara ya Bahi Mkoani Dodoma na kupongeza Mkoa kwa kutekeleza mradi rafiki wa mfano kwa wamachinga wa mkoa huo kupitia fedha za ndani.
Waziri Bashungwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshatoa bilioni 5 kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajiri ya kuboresha miundombinu na kuweka mazingira wezeshi ya Wafanyabiashara Wadogo (Machinga) nchini ambapo milioni 500 zimeletwa Dodoma Jiji.
Aidha, Waziri Bashungwa ameeleza Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI inaendelea kuwasiliana na wadau wa maendeleo na sasa ipo katika mazungumzo na Serikali ya India ili kuweza kupata fedha za kuongeza kwenye bilioni 5 zilizotolewa na Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwaajiri ya Wafanyabiashara wadogo.
Waziri Bashungwa ameeleza kuwa tarehe 14 mwezi Machi 2022 amewaita Wakuu wa Mikoa wanaotoka kwenye majiji waambatane na Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Wakurugenzi ili kujadili na kupanga namna bora ya kujenga masoko ya wazi ya kisasa yatayoleta mageuzi makubwa kwa Wafanyabiashara Wadogo nchini.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema mradi huo utakapokamilika mwezi mei, machinga wote walioko katika maeneo ya jiji la Dodoma watahamishiwa kwenye eneo hilo rasmi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.