HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepanga kujenga majengo saba yenye ukubwa tofauti ikiwemo hoteli ya kisasa itakayokuwa na ghorofa 11 na vyumba 117 katika eneo lilipo jengo la ‘Paradise’ kwa sasa, katikati ya Jiji hilo itakayojulikana kama ‘Dodoma City Hotel’.
Mbali ya hoteli hiyo, Halmashauri hiyo pia itajenga jengo lenye ghorofa pacha jirani na viwanja vya Nyerere litakalojulikana kama ‘Nyerere Square Plaza’ huku Government City Complex’ litakalokuwa na ghorofa sita likijengwa katika eneo la Mtumba ulipo Mji wa Serikali.
Akizungumza wakati wa Baraza Maalum la Madiwani wa Halmashauri hiyo jana Jijini humo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alisema wamepanga kujenga miradi hiyo mikubwa kimkakati na kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri ili iwe vyanzo vya kudumu vya Halmshauri hiyo iliyolenga kujitegemea na kujiendesha kwa mapato yake kabla ya mwaka 2025.
Kunambi alisema majengo mengine ni pamoja na ‘Dodoma City Complex’ litakalokuwa na ghorofa nne na litajengwa katika eneo la Dodoma Makulu Barabara ya kuelekea Chuo Kikuu cha Dodoma, ambapo pia kutajengwa jengo jingine la ‘Apartments’ katika eneo hilo.
“Mradi mwingine itakuwa ni ‘Nunge Investment’ ambalo litakuwa jengo la ghorofa 9, huku likiwa na migahawa mingi ya kisasa ndani yake” alisema Kunambi mbele ya wajumbe wa Baraza hilo lenye Madiwani 60.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Halmashauri hiyo itajenga jengo lingine litakaloitwa ‘Dodoma City Plaza’ katika eneo ambapo kuna ukumbi wa ‘NK’ Jijini humo na kufanya Jiji kuwa na majengo saba yatakayotoa huduma mbalimbali kama malazi, vyakula, makazi, Ofisi na kumbi za mikutano.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko tayari na tunaanza sasa…tutasaini mikataba ya ujenzi kabla ya Julai 5, 2019 kwa ajili ya majengo mawili ya Dodoma City Hotel na lile la Government City Complex litakalokuwa ndani ya Mji wa Serikali pale Mtumba…haya majengo mawili tunayajenga kwa fedha zetu za mapato ya ndani ya Halmashauri” alisisitiza Kunambi.
Alisema miradi mingine itajengwa kwa kuomba fedha Serikali Kuu kupitia miradi ya kimkakati, na mingine itajengwa kwa Halmashauri kukopa fedha katika mabenki.
Mkurugenzi Kunambi alisema miradi hiyo itakuwa na tija kubwa ikiwemo kuongeza mapato ya Halmashauri, kuongeza ajira kwenye Jamii, kuufanya Mji wa Dodoma kuvutia na kuongeza ujio wa watalii na wageni wengine. Aidha miradi hii itasaidia Jiji kupunguza utegemezi kutoka Serikali Kuu, na kuvutia wawekezaji.
Wajumbe wa Baraza hilo wakiongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Mstahiki Meya Prof. Davis Mwamfupe walielezea kuvutiwa na miradi hiyo huku wakishauri ujenzi wake ukamilike kwa wakati ili iwe na tija na kufikia malengo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.