Vituo vya Huduma Pamoja (One Stop Service Center) vya awali vimeanza kufanya kazi tangu tarehe 01 Julai, 2021 katika majiji ya Dar es Salaam na Dodoma na vyote viko katika majengo ya matawi ya Shirika la Posta Tanzania.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni miongoni mwa taasisi za mwanzo kabisa ambazo zimeanza kutoa huduma katika Kituo cha Huduma Pamoja Dodoma, ambapo Afisa Biashara Mwandamizi wa Jiji la Dodoma ametolea maelezo kuhusiana na huduma wanazozitoa ili kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa huduma.
Afisa Biashara Mwandamizi wa Jiji la Dodoma, Donatila Vedastus (pichani juu) amesema kuwa, “Katika Kituo cha Dodoma tunatoa fomu za maombi ya leseni za biashara, tunatoa elimu inayohusiana na uendeshaji wa biashara kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Aidha, tunatoa namba za malipo (Control Number) kwa ajili ya malipo ya serikali ya leseni za bishara na vileo, pia tunasajiri wafanyabiashara wapya kwenye mfumo wa ukusanyaji wa mapato na kuhuisha leseni za biashara zilizoisha muda wake”. Amesema Afisa huyo wa Jiji la Dodoma na kutoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara wa Dodoma kufika katika kituo hicho ili kupata huduma.
Vedasto ameishukuru Serikali kwa kuliona hili la kufungua Kituo cha Huduma Pamoja, “Sisi kama Jiji tumepata eneo la ziada la kutolea huduma zetu, hapo mwanzo tulikuwa tunatoa huduma hizi kwenye ofisi zetu zilizoko karibu ya Sabasaba pekee, lakini sasa tuna mahali pengine na wafanyabiasha wamepata uwanja mpana wa kuchagua mahali palipo karibu kwao kufika na kupata huduma zile zile kwa urahisi zaidi. Lakini, imesaidia kupunguza msongamano na foleni kwa wateja wetu” alimalizia Afisa huyo Mwandamizi.
Naye Waziri Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amesema kwenye ukurasa wake rasmi wa ‘twitter’ kuwa, “Chini ya ‘Huduma Pamoja’, huduma za BRELA, RITA, NIDA, Uhamiaji, NSSF, PSSSF na nyinginezo zitakuwa zinapatikana kwenye matawi ya Posta nchini. Tumeanza na Dar es Salaam na Dodoma na tunakusudia kueneza huduma hizi nchi nzima.”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.