Na Nemes Michael, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeendelea kutekeleza kaulimbiu ya wiki ya mazingira duniani isemayo “Tutumie nishati mbadala ili kuongoa mfumo ikolojia”, kwa kutoa elimu ya mazingira na jinsi ya kuyahifadhi katika banda la maonesho kuelekea kilele cha siku ya Mazingira Duniani katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini humo.
Akizungumzia maadhimisho hayo yanayoendelea duniani kote, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Ally Mfinanga alisema kuwa, wamefanikiwa kuungana na wadau mbalimbali wanaohusika katika sekta ya mazingira kuhakikisha wanatoa elimu kwa wakazi wote wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla hususan wale watakaotembelea mabanda ya maonesho hayo kwani kuna wataalam mbalimbali wanaotoa elimu ya utunzaji wa mazingira na jinsi ya kukabiliana na athari za tabia ya nchi.
“Tunatumia fursa hii kuhamasisha wakazi wote wa Jiji la Dodoma katika upandaji miti, na ndiyo njia sahihi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, lakini pia nasisitiza matumizi ya nishati mbadala ili kuweza kuokoa mfumo wa ikolojia” alisema Mfinanga.
Mfinanga aliongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweka mikakati endelevu katika kuhakikisha maendeleo ya utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati mbadala.
Kwa upande wake, mhasibu wa kikundi cha GRK Group Tanzania ambaye pia ni mjasilimali Pendo Kasogota alisema kuwa kaulimbiu inayotumika inatukumbusha umuhimu wa mazingira katika maisha yetu ya kila siku.
“Kaulimbiu ya wiki ya mazingira inatukumbusha kutambua umuhimu wa mazingira hivyo, yatupasa kuyatunza, kuyapenda na kuyaheshimu mazingira lakini pia maadhimisho haya yanatusaidia wajasiliamali wadogo katika kuonekana hata kufahamika” alisema Kasogota.
Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yanafanyika kitaifa jijini Dodoma kuanzia tarehe 1 Juni hadi tarehe 5 Juni, 2021 katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Mrisho Kikwete ambapo mgeni rasmi katika ya kilele anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.