HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepanga kuendeleza bwawa la Zuzu ili kuwa na tija kwa wakazi wa Jiji hilo kwa kuwahakikishia lishe bora na kuongeza mapato ya ndani.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Gratian Mwesiga alipowasilisha taarifa ya bwawa la Zuzu kwa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma walipotembelea bwawa hilo.
Mwesiga alisema kuwa kutokana na umuhimu wa bwawa hilo, katika mwaka wa fedha ujao, Halmashauri itashirikiana na wadau na kuangalia mpango wa kuendeleza bwawa hilo. Aliongeza kuwa bwawa hilo ni muhimu kwa sababu linawawezesha wananchi kupata uhakika wa lishe bora. Bwawa hili likiendelezwa litaiwezesha Halmashauri pia kupata mapato ya ndani.
Akiongelea samaki katika bwawa hilo, Mkuu huyo wa idara alisema samaki waliomo kwenye bwawa hilo waliletwa na maji ya mvua kutoka kwenye mabwawa ya wafugaji wa samaki walio maeneo ya jirani baada ya mabwawa hayo kufurika. “Samaki hawa waliingia kama mayai au vifaranga ambao wameendelea kukua na kuzaliana. Samaki wanaopatikana kwenye bwawa hili ni Kambale na Perege. Mpaka sasa bwawa hili lina jumla ya wavuvi 15. Wavuvi wote hawa wamelipa leseni ya uvuvi kwa mwaka 2021” alisema Mwesiga.
Akiongelea jinsi bwawa hilo lilivyoanza, alisema kuwa lilianza kama mbuga kwa miaka mingi na wakazi wa eneo hilo waliitumia kulima mpunga. “Zamani kwenye mbuga hii kulikuwa na miti mingi hivyo, maji yalikuwa yanatuama na kukauka. Baada ya kukata miti, maji hayakuendelea kutuama kwa muda mrefu, yalijaa wakati wa mvua na baadae kukauka” alisema Mwesiga.
Maji katika bwawa hilo yalianza kujaa tangu mwaka 2018 na yameendelea kuongezeka hadi mwaka 2021 na samaki wameanza kupatikana mwanzoni mwa mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Dodoma Meja Mst. Johnick Risasi alisema kuwa kamati yake imefurahia kuona wakazi wa Kata ya Zuzu wakinufaika na bwawa hilo na kuishauri halmashauri kufikiria namna na kuliendeleza bwawa hilo ili liwe na tija zaidi kwa wananchi na kuiwezesha halmashauri kupata mapato.
Nae Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma, Sophia Kibaba alishauri kuwa kina cha bwawa hilo kiongezwe ili kuongeza uhakika wa upatikanaji Samaki.
Bwawa la Zuzu lipo Tarafa ya Zuzu, Kata ya Zuzu likigusa mitaa ya Pinda, Chididimo, Sokoine na Mtaa wa Bihawana katika kata ya Mbabala na Mtaa wa Michese kata Mkonze.
Muonekano wa Bwawa la Zuzu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.