Na Josephina Kayugwa, DODOMA
MGANGA Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method, amewataka Maafisa Lishe kushirikiana na viongozi wa Kata pamoja na Mitaa kuendelea kutoa elimu kwa wamama wajawazito pamoja na wananchi wote kujua umuhimu wa kuwahi kliniki kwaajili ya kujua maendeleo ya kiafya pamoja na kutumia vyakula vyenye lishe ili kuondoa udumavu na utapiamulo mkali.
Dkt. Andrew ameyasema hayo katika kikao cha tathimini ya mkataba wa lishe ngazi ya Kata robo ya kwanza Julai – Septemba 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Alisema kuwa suala la lishe bora ni jambo la muhimu ambalo kila mwananchi anatakiwa kulijua kwasababu wajawazito wengi wamekuwa hawahudhurii hospitali lakini pia wengi wao hawatumii vyakula vya lishe kitu ambacho kinawaletea matatizo wakati wa kujifungua.
“Kinamama wote wanatakiwa wapatiwe elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa lishe pamoja na kwenda kliniki wakati wote wa ujauzito ili kuondokana na haya matatizo, maana wajawazito wamekuwa wakipoteza damu nyingi au kupoteza maisha wakati wa kujifungua.
Inatakiwa kama wataalamu wa afya tuhakikishe jambo hili la kutoa elimu katika Kata na Mitaa yetu linafanikiwa kwa kiasi kikubwa maana hata kama mama atajifungua salama kama hatumii lishe basi mtoto atakuwa na utapiamulo mkali pamoja na udumavu,” alisema Method.
Kwa upande wake Afisa Lishe Jiji la Dodoma, Semeni Juma, alisema katika kupambana na tatizo la utapiamulo jijini la Dodoma linakwisha, uongozi wa Kata na mitaa kwa kushirikiana na wahudumu wa ngazi ya jamii wanatakiwa kuendelea kufanya ufuatiliaji wa watoto walioibuliwa wenye utapiamulo mkali kwenye mitaa na kuhakikisha siku ya afya na lishe inafanyika kwa kila mtaa.
“tunatakiwa kuondoa tatizo la utapiamulo mkali kwa watoto wetu kwa kuhakikisha watendaji wanasimamia vyema uwepo wa program za uzalishaji wa chakula kwa wanafunzi katika shule zote za msingi na sekondari zilizopo kwenye kata.
Pia, katika vituo vyote vya afya kuwepo namba za watendaji wa Kata ili kupata taarifa za watoto wenye utapiamulo, hii itasaidia kujua jinsi gani ya kutatua tatizo hili lakini pia chumvi ambayo inatumika inatakiwa kupimwa ili kujua kama ina madini joto ndipo itumike,” alisema Semeni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.