HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inatarajia kufikia lengo la asilimia 100 ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua Rubella na Polio kutokana na ziara ya tathmini iliyofanyika leo.
Kauli hiyo ilitolewa na mganga mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Gatete Mahava alipofanya ziara ya kukagua hali ya zoezi la chanjo ya kitaifa inayoendelea.
Katika majumuisho ya ziara hiyo, yaliyofanyika katika kituo cha Village of Hope kilichopo jijini hapa, Dkt. Mahava alisema “Leo siku ya Jumamosi tarehe 19/10/2019 muitikio wa wananchi kupeleka watoto katika vituo vya chanjo ni mzuri na wananchi wanaendelea kuwaleta watoto kupatiwa chanjo ya Surua Rubella na Polio. Na kama tulivyoshuhudia katika vituo tulivyopita, idadi imeendelea kuongezeka ikilinganishwa na siku zilizotangulia”. Mganga huyo alionesha kuridhishwa na zoezi la chanjo katika Halmashauri hiyo. Kutokana na hamasa inayoendelea kutolewa kupitia matangazo mbalimbali na ushuhuda wa wananchi ambao watoto wao wamepatiwa chanjo, Halmashauri ya Jiji itafikia asilimia 100 ya lengo, aliongeza.
Akiongelea hali ya zoezi la chanjo ya Surua Rubella na Polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, muuguzi mkunga wa kituo cha Village of Hope, Eleonilla Missanya alisema kuwa muitikio ni mzuri. “Siku ya kwanza muitikio ulikuwa kidogo lakini hamasa inavyoendelea, watu wanaendelea kuleta watoto wao kupatiwa chanjo. Siku ya kwanza tulichanja watoto 145, siku ya pili 172 na leo hadi saa 7 mchana tumechanja watoto 253” alisema Missanya.
Katika ziara ya ufuatiliaji iliyofanywa na Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, vituo vinne vilitembelewa. Vituo hivyo ni Kituo cha Afya Makole, zahanati ya Makole, kituo cha NESUDA na kituo cha Village of Hope.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.