HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati Tanzania (TSCP) limetoa Pikipiki tatu za Magurudumu Matatu (Toyo) na vifaa vya kutunzia uchafu vyenye thamani ya shilingi Milioni 28.4 kwa vikundi vitatu vinavyofanya kazi za uzoaji taka ngumu kwenye makazi na maeneo ya biashara, ikiwa ni juhudi za kuimarisha usafi na usimamizi wa taka ngumu katika jiji hilo.
Makabidhiano ya pikipiki hizo yamefanywa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge kwa vikundi vitatu ambavyo ni Dodoma Youth Environmental Care and Sanitation Group ambacho kinafanya kazi zake katika Kata ya Kizota, Mshikamano Group - Nzuguni C ambacho kinafanya kazi zake katika Kata ya Nzuguni pamoja na Kikundi cha Soft Chivwele Group ambacho kinafanya kazi katika Kata ya Miyuji.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Dkt Mahenge alipongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi katika kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa katika Mazingira safi na salama.
“Jambo la kwanza ni kukupongeza Mkurugenzi kwa kazi nzuri unayofanya. Katika karne hii ya 21 majiji ya kisasa ni lazima yaongozwe na usafi na sisi tuna bahati kwamba tumepata fursa hiyo ya kujenga Makao Makuu ya nchi kwenye karne hii ya 21 ambayo imejaa teknolojia za kisasa, kwa hiyo tukitumia vizuri teknolojia tutakuwa na jiji la kisasa kuliko majiji mengine duniani” Alisema Dkt. Mahenge.
Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza vikundi hivyo kuwa wasitumie pikipiki hizo kufanya biashara nyingine tofauti na kazi ya uzoaji taka katika kata mbalimbali za Halmshauri ya Jiji hilo.
Aidha, Dkt. Mahenge alipiga marufuku kufanya shunguli za kilimo na ufugaji katikati ya mji, na kudai kuwa, Jiji katika mipango yake limeainisha maeneo mahsusi kwa ajili ya kufanya kilimo na ufugaji hivyo ni kosa kufanya shughuli hizo katikati ya Mji.
“Dodoma tunayo ardhi ya kutosha kufanya kilimo na ufugaji nje ya eneo la Makao Makuu ya nchi, ufugaji katikati ya mji unaweza kusababisha ajali, kwa hiyo ni marufuku na nimekwisha waagiza viongozi wote wanaohusika” alisisitiza Dkt. Mahenge.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, aliwataka wakazi wa jiji hilo kushirikiana kwa karibu na Halmashauri ili kuhakikisha mazingira yote yanakuwa safi, na kwamba wajenge utamaduni wa kutoa fedha za tozo ya uzoaji taka kwa ajili ya kuviwezesha vikundi hivyo kufanya kazi hiyo ya uondoshaji taka kwa ufanisi mkubwa.
Akiwasilisha changamoto hiyo ya michango kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Kunambi alisema kuwa, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Halmashauri yake katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, lakini bado kuna baadhi ya wananchi na taasisi hazitoi ushirikiano kwa kutoa tozo za uzoaji taka.
“Napenda Wananchi watambue kuwa, haya magari yanawekwa mafuta, na gharama za uendeshaji wake ni kubwa, hivyo ni lazima wachangie, bado tunachangamoto ya kulipia kwenye kaya na kwenye baadhi ya taasisi…hatuwezi kuwa na mji safi kama wananchi hawachangii. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na wenzetu wa ‘Green Waste’ tunawakumbusha wananchi kuchangia zoezi hili kwa sababu kusafisha jiji ni jukumu letu sote” alisema Kunambi.
Hata hivyo, Kunambi alitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuwa magonjwa mengi yanatokana na uchafu na hivyo kuwaomba wananchi kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuweka mazingira safi.
Naye Kaimu Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ally Mfinanga alivitahadharisha vikundi vyote kuwa pikipiki hizo zinapaswa kuwa katika hali nzuri katika kipindi chote cha matumizi na kuvikumbusha kuwa vitawajibika kulipa kodi stahiki za Serikali zinazohusiana na uendeshaji wa pikipiki za magurudumu matatu.
“Vikundi vyote vitawajibika kulipa kodi, kufuata sheria, kanuni, na taratibu za uendeshaji wa vyombo vya moto na usalama barabarani, na niongeze kwa kusema kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma au mwakilishi wake atakuwa na haki ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa pikipiki hizi pasipo kutoa taarifa kwa kikundi husika” alisema Mfinanga.
Alivitaka vikundi vyote kufungua akaunti Benki itakayotumika kuweka fedha za matengenezo ya pikipiki hizo angalau kiasi kisichopungua laki moja na nusu kwa mwezi na risiti ya fedha hizo kuwasilishwa katika Ofisi ya Mkurugenzi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.