HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma ipo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa madarasa mapya 37 na kukarabati madarsa mengine saba huku ukamilishaji wa maabara nao ukiendelea kwa kasi ili madarasa yaliyokua yanatumika kama maabara katika shule nyingi yabaki kwa matumizi ya madarasa.
Mkurugenzi wa jiji Godwin Kunambi amesema hatua za haraka zilichukuliwa na jiji la Dodoma kutokana na upungufu wa madarasa takribani 52 na kupelekea jumla ya wanafunzi 2,610 kukosa nafasi za kujiunga kidato cha kwanza hapa Jijini.
Katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma mwanzoni mwa mwezi huu, Kunambi alibainisha mikakati hiyo ya ujenzi wa madarasa ilivyofanyika kwa haraka ambapo katika kuhakikisha ufanisi na ubora uliokusudiwa unapatikana, alifanya kikao na Wakuu wa Shule wote na kupanga mpango mkakati wa usimamizi wa ukamilishaji wa ujenzi huo.
Aidha Kunambi ameeleza kuwa, kila Mkuu wa Idara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alikabidhiwa Shule kwa ajili ya kusimamia ili ujenzi ufanyike kwa haraka na ufanisi ikiwa ni pamoja na kuzingatia taratibu stahiki za ujenzi na manunuzi.
Akielezea siri ya mafanikio hayo ya ujenzi yaliyochukua takribani mwezi mmoja tu, Kunambi alisema amepata ushirikiano kutoka kwa Wakuu wa Shule, Watendaji, na Madiwani, huku akitoa wito kwa wadau wote kuendeleza mshikamano huo ili kuwaletea maendeleo Wakazi wa Jiji la Dodoma.
"Jiji la Dodoma limekua na ongezeko kubwa la watu kutokana na kuwa na wakazi wengi wanaohamia Dodoma kikazi kwa kuwa Serikali yote inahamia Dodoma kwa sasa, hivyo mahitaji ya miundombinu katika sekta mbalimbali yanaongezeka sana" amefafanua Kunambi.
Maeneo mbalimbali katika Kata zote za Jiji la Dodoma yanaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali kama ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa matundu ya vyoo, ujenzi wa maabara, ujenzi wa madarasa, hosteli, nyumba za walimu, ujenzi wa masoko na majengo ya ofisi za Kata na Ofisi za Shule.
Baadhi ya Kata zilizotembelewa na kukuta miradi mbalimbali ikitekelezwa ni pamoja na Mtumba, Hombolo, Ihumwa, Kikombo, Nzuguni, Ipagala, Dodoma Makulu, Kilimani, Ntyuka, Mkonze, Mpunguzi, Mbabala, Zuzu, Chigongwe, Msalato, Mnadani, Kiwanja cha Ndege, Mbalawala, Nala, Viwandani na Nkuhungu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.