HALMASHAURI ya jiji la Dodoma imetoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika utekelezaji wa Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019 za Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa inavyoelekeza kila Halmashauri kutenga asilimia 10 ya fedha zake za mapato ya ndani kwa ajili ya makundi hayo katika jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utoaji mikopo isiyo na riba kwenye hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi 1,062,500,000 ambayo imefanyika katika uwanja wa Nyerere Square jijini hapa mbele ya mgeni rasmi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo.
Kunambi amesema kuwa fedha za vikundi zinazokabidhiwa leo kiasi cha shilingi 1,062,500,000 zinaifanya Halmashauri ya Jiji kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kutoa mikopo ya jumla ya shilingi 2,859,230,000 sawa na asilimia 109.6 ya lengo. Vikundi vya wanawake 125 vimekabidhiwa jumla ya shilingi 626,000,000, wakati vikundi 73 vya vijana vimekabidhiwa shilingi 419,000,000 na vikundi vitatu vya watu wenye ulemavu vimekabidhiwa shilingi 17,500,000.
Akifafanua zaidi Mkurugenzi Kunambi amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kiasi cha shilingi 2,606,645,760 zilitengwa katika bajeti ya Halmashauri ambapo shilingi 1,796,730,000 zilitolewa katika kipindi cha kuanzia mwezi wa Julai hadi Disemba, 2018 na vikundi kunufaika. Marejesho ya mikopo hiyo yamefikia kiasi cha shilingi 311,853,517 na muda wa marejesho unaendelea, alisisitiza Kunambi.
Aidha, aliongeza kuwa vikundi 1,020 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilikwisha nufaika na mikopo ya Halmashauri ya jiji hilo vikiwa na mzunguko wa shilingi 3,497,257,316.33.
Vile vile Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka ujao wa fedha 2019/2020 imetenga shilingi 3,392,614,798 katika bajeti yake ya kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Miongoni mwa vikundi vilivyonufaika na mikopo hii ni kikundi cha vijana watano waliohitimu Chuo Kikuu cha Dodoma na kuanzisha kikundi chao kinaitwa "Tanzania Wazalendo Youth Group". Vijana hawa wajasirimali wamejiajiri kwa kufanya biashara ya kuuza 'Juice'. Kikundi chao kimepewa mkopo usio na riba wa kiasi cha shilingi milioni 10.
Aidha, akizungumza kwa niaba ya vijana wenzie, Joel William alisema kuwa "...leo tumepata milioni 10, na tuna miaka sita mpaka kumaliza utawala wa rais Magufuli. Mpango wetu ni kupata milioni 60, yaani milioni kumi kila mwaka. Lakini tulisikia kama utakuwa mtendaji mzuri katika kurejesha, basi utakuwa na nafasi ya kupata mkopo mkubwa zaidi.
Hivyo basi, tunalo lengo la kufikia mpaka milioni 70 ili kama alivyosema Mheshimiwa Jafo kuwa tuwe matajiri, kwa hiyo, mpaka rais Magufuli atakapotoka madarakani aseme kuna kikundi Dodoma kinaitwa "Tanzania Wazalendo Youth Group" ni mfano wa vijana niliowasaidia na sasa ni matajiri". Amesema Joel kwa kujiamini huku akiipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa utekelezaji wa malengo iliyojiwekea kuwasaidia wananchi wake.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.