HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mtumishi wake Marehemu Hellen Minja aliyefariki tarehe 7 Septemba, 2020 katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Akitoa salamu za Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana wa Jiji hilo, Sharifa Nabalang’anya nyumbani kwa Marehemu eneo la Nkuhungu jijini hapa, alisema msiba huo ni pigo kubwa kwa Halmashauri hiyo.
“Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji alitamani sana kushiriki nasi katika misa hii, lakini kwa bahati mbaya anamajukumu mengine ya kiserikali. Kwa hiyo sisi watumishi wa Jiji tupo hapa kwa niaba yake, anatoa pole kwa wafiwa wote kutokana na msiba huu. Sisi kama Jiji la Dodoma tumesikitishwa sana na msiba huu, kwa sababu tumepoteza kiungo muhimu sana miongoni mwa watumishi wetu” alisema Nabalang’anya.
Alisema kuwa Halmashauri imechangia uwezeshaji wa misa ya kumuaga marehemu na kugharamia usafiri na sanduku lililohifadhi mwili wa marehemu. “Lakini pia tuna kiasi cha shilingi 479,000 na michango mingine ofisini inaendelea na tutakaporudi kutoka msibani tutaiwasilisha. Kama Jiji, tutumie fursa hii kuwaombea wasafiri wote wanaoenda Marangu safari njema, nasi tutatuma wawakilishi wetu huko Marangu. Kipekee tumuombee mwenzetu apumzike sehemu salama, Bwana alitoa na Bwana ametoa jina lake lihimidiwe” aliongeza Afisa Maendeleo ya Jamii huyo machozi yakimlenga.
Kwa upande wake Afisa Nyuki wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Evarist DeSouza alimtaja Marehemu Hellen Minja kuwa alikuwa ni mtumishi muadilifu na mchapa kazi. “Nasikitika sana kutokana na kifo cha mwenzetu Mama Minja, tumuombee heri katika safari yake aliyoianza, Mwenyezi Mungu ampokee na tuendelee kumuombea. Utumishi wake katika Halmashauri ulikuwa wa kuigwa. Nashukuru alikuwa ni mtumishi muadilifu, muelewa na mchapakazi” alisema DeSouza kwa huzuni kuu.
Akiongelea alama aliyoacha, alisema kuwa Idara aliyokuwa anaisimamia ya Maendeleo ya Jamii na Vijana ilionekana katika kuwasaidia vijana na wazee. Atakumbukwa kwa kupigania maslahi ya watumishi walio chini yake, aliongeza.
Akisoma wasifu wa Marehemu Hellen Minja, Patrick Sebyiga alisema kuwa marehemu alizaliwa tarehe 19 Disemba, 1962 Dareda Babati. Marehemu Hellen Minja alipata elimu ya msingi katika shule ya Dareda na kuhitimu mwaka 1976. Elimu ya sekondari alipata katika shule ya sekondari ya wasichana Machame na kuhitimu mwaka 1980. Mwaka 1983 alihitimu kitado cha sita katika shule ya wasichana ya Zanaki, aliongeza.
Mwaka 1984 alipata mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa katika kambi ya Mafinga & Lua iliyopo Mkoani Iringa. Mwaka 1987 alihitimu Stashahada ya Juu katika fani ya Maendeleo ya Jamii Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tengeru kilichopo Mkoani Arusha.
Sebyiga alisema kuwa mwaka 1988, Marehemu aliajiriwa katika Utumishi wa Umma na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kwa cheo cha Afisa Maendeleo ya Jamii II na kituo chake kikiwa Kata ya Hombolo. Kutokana na utendaji wake wa kazi alifanikiwa kupandishwa vyeo kwa vipindi tofauti tofauti, alisema. Mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Mwaka 2007 alihamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuendelea na wadhifa huo, aliongeza Sebyiga. Marehemu mpaka mauti inamfika alikuwa mtumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana.
Marehemu alifunga ndoa na Felix Minja tarehe 20/12/1986, wamebahatika kupata watoto wanne wakiume, alisema.
Akiongelea ugonjwa wa Marehemu, alisema kuwa marehemu alianza kuugua mwaka 2017. Marehemu alitibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Benjamini Mkapa, DCMC, Hospitali ya Dr. Kinabo Medical Avenue, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Regency – Dar es Salaam.
“Marehemu alifariki 07 Septemba, 2020 saa 8:15 mchana wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma. Marehemu ameacha Mgane, watoto wanne wakiume na wajukuu watano. Tunapenda kutoa shukrani kwa Madaktari na Wauguzi wote wa Hospitali alizokuwa akitibiwa Marehemu, kwa jitihada walizozifanya za kuokoa maisha ya mpendwa wetu. Pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alisema Sebyiga kwa huzuni kubwa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Sharifa Nabalang'anya akitoa salam za Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Sharifa Nabalang'anya akikabidhi mchango wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mume wa marehemu Felix Minja.
Picha na matukio waombolezaji wakati wakitoa heshima za mwisho kwa marehemu Hellen Minja (hapa chini).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.