HALMASHAURI ya jiji la Dodoma imepeleka shilingi bilioni saba Serikali kuu zaidi ya mara mbili ya fedha iliyopangiwa kukusanywa katika kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akielezea hali ya utekelezaji wa shughuli za sekta ya Ardhi kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angelina Mabula aliyefanya ziara ya kikazi jijini hapo jana.
Kunambi alisema “Kwa upande wa mapato, mwaka jana shilingi bilioni saba tumepeleka Serikali kuu, kati ya lengo la shilingi bilioni tatu tulizopangiwa”.
Makusanyo hayo yanatokana na kodi ya pango la ardhi pamoja na maduhuli mengine kwa mwaka wa fedha 2017/2018, aliongeza.
Aidha, alieleza kuwa maduhuli hayo yanatokana na ada za uandaaji hati, ada ya uhuishaji hati, ada za uhamisho wa milki, ushuru wa stempu na malipo ya mbele.
Akizungumzia upimaji na uuzaji wa viwanja, Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu Halmashauri ya jiji hilo imepima na kuuza viwanja 45,869. “Shukrani kwa wataalam wa Idara ya Ardhi kwa kazi nzuri, kwa kipindi kifupi tumeweza kupima na kuuza viwanja vingi” alisema Kunambi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angelina Mabula alifanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kukagua utekelezaji wa shughuli za sekta ya Ardhi na kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.