HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeongeza uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 13 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 katika jihudi zake za kujitegemea kimapato.
Kauli hiyo ilitolewa na katibu wa Baraza la Madiwani ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kukamilika kwa ufungaji hesabu za Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwenye mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupitia hesabu za mwaka wa fedha 2018/2019 katika ukumbi Mikutano wa Halmashauri.
Kunambi alisema kuwa uwezo wa Halmashauri kujitegemea umepanda kwa asilimia 13. “Mheshimiwa Mwenyekiti, hesabu zetu za mwaka 2018/2019 zinaonesha kuwa, uwezo wa kujiendesha kwa kutumia mapato ya ndani umepanda kutoka asilimia 34 ya mwaka uliopita hadi kufikia asilimia 47. Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia ya uwezo wa kujitegemea unakokotolewa kwa kulinganisha jumla ya mapato ya ndani na matumizi yote ya Halmashauri kwa mwaka husika” alisema Kunambi. Matumizi yanayolinganishwa yanajumuisha fedha za mapato ya ndani, ruzuku ya mishahara, miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na serikali, wahisani pamoja na matumizi mengineyo, alisema Kunambi.
Akiongelea uwezo wa Halmashauri kulipa madeni, Kunambi alisema kuwa uwezo wa kulipa madeni kwa mwaka 2018/2019 umeongezeka kutoka uwiano wa 1.5:1 ya mwaka uliopita hadi 2.6:1 mwaka huu, alieleza. “Ukokotoaji wa uwiano hufanyika kwa kuchukua jumla ya thamani ya mali za muda mfupi tulizonazo na kugawanya na jumla ya madeni yote ya muda mfupi” alisema Kunambi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma mjini, Robert Mwinje amepongeza mkutano huo, na kuutaja kuwa mkutano mzuri. “Kipekee taarifa hii tuliipata mapema na kuipitia. Mimi kitaaluma ni mhasibu, hongera sana mkurugenzi wa jiji kwa taarifa nzuri. Waheshimiwa madiwani hakuna taarifa iliyofichwa” alisema Mwinje. Taarifa inaonesha uwezo wa halmashauri kukua mwaka hadi mwaka, hili ni jambo zuri la kujivunia.
Akichangia hoja katika kikao hicho Diwani wa kata ya Chang’ombe kupitia Chama cha Mapinduzi Mhe. Bakari Fundikira amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumwamini na kumteua Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwani amekua chachu ya maendeleo katika Jiji hilo kutokana na ufanisi wake mkubwa katika kazi hasa katika kuiwezesha Halmashauri kujitegemea kutokana na mapato yale ya ndani.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi alipongeza kwa uwasilishaji mzuri wa taarifa ya kukamilika kwa ufungaji hesabu za Halmashauri kwa mwaka 2018/2019.
Diwani wa kata ya Chang’ombe kupitia Chama cha Mapinduzi Mhe. Bakari Fundikira akichangia hoja kwenye Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dodoma kupitia taarifa ya kukamilika kwa ufungaji hesabu za Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Katibu wa Baraza la Madiwani ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma akitoa ufafanuzi wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ya Hesabu za kufunga mwaka za Halmashauri ya Jiji la Dodoma mbele ya madiwani na wataalam wa jiji la Dodoma (hawapo pichani). Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Patrobas Katambi na katikati ni Naibu Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Emmanuel Chibago.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.