HALMASHAURI ya jiji la Dodoma imeongeza uwezo wake wa kujitegemea kwa kutumia mapato ya ndani kutoka asilimia 9 za awali hadi kufikia asilimia 34 kwa mujibu wa taarifa ya hesabu za Fedha kwa mwaka ulioishia Juni 2018.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Godwin Kunambi kwenye mkutano wa wazi wa baraza la madiwani wa robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha.
Kunambi amesema kuwa, hadi sasa jumla ya shilingi billioni 14 zimeshakusanywa na Halmashauri ya Jiji ambapo lengo lake ni kuhakikisha inakusanya jumla ya shilingi bilioni 67 katika mwaka wa fedha 2018/2019 kama Halmashauri hiyo ilivyojipangia.
“Halmashauri ya jiji la Dodoma ndio Halmashauri inayoongoza kwa kujitegemea ikifuatiwa na halmashauri ya Manispaa ya Ilala iliyopo jiji la Dar es Salaam” alifafanua.
“Mpaka sasa Halmashauri ya Jiji la Dodoma endapo itajitegemea yenyewe bila kupokea fedha kutoka serikali kuu inaweza kujiendesha kwa muda wa miezi mitano” alisema Kunambi.
Wajumbe wa mkutano huo wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe wamepongeza hatua ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupiga hatua katika makusanyo na kushauri juhudi zaidi ziongezwe ili kutimiza malengo ya makusanyo iliyojiwekea kwa mwaka huu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.