HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imewataka wafanyabiashara wote wasio na mikataba ya pango kwenye masoko ya Jiji kufika katika Ofisi za Jiji hilo kwa ajili ya kupatiwa mikataba halali wanayotakiwa kuwa nayo kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Masoko wa Jiji James Yuna alipokuwa akibainisha changamoto zinazowakabili wakati wa kusimamia makusanyo ya tozo za vibanda vya biashara.
"Imekuwa ni kawaida baada ya mkataba wa awali kuisha wafanyabiashara wamekuwa wakifika ofisini na kuchukua mikataba, lakini baadaye tumeona kuna mwitikio mdogo sana wa kuja kuchukua mikataba, tunatoa rai kwa wafanyabiashara wa masoko yetu yote wanaohusika na mikataba wafike ofisini, waijaze ili taratibu nyingine ziweze kuendelea" alisema James Yuna.
Kumekuwa na tabia ya wafanyabiashara kujisahau baada ya kupewa vibanda na kujikuta wanapata usumbufu mkubwa katika kuendesha biashara zao pale mikataba hiyo inapohitajika. Kuhusu wafanyabiashara wanaopanga bidhaa za vyakula kandokando ya barabara, Yuna amesema ni hatari sana kuweka bidhaa barabarani kwa kuwa bidhaa kama nyanya na vitunguu kiafya si salama na ni hatari, pia kumekuwa na ajali mbalimbali ambazo waathirika wakubwa ni wafanyabiashara waliopo barabarani.
Aidha, Halmashauri kupitia kitengo cha masoko wanatarajia kuanzisha mpango wa elimu kwa wafanyabiashara wote na wadau wa masoko ili waweze kutambua faida za kuwa na mikataba na hasara za kutokuwa mikataba lakini pia kuwaeleza juu ya faida na hasara za kutokuwa kwenye masoko rasmi na mambo mengine yanayohusiana na masoko.
Tembelea ukurasa wetu wa Youtube (Dodoma City TV) kumsikiliza Afisa Masoko wa Jiji, au bofya hapa:Onyo kwa wasio na mikataba
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.