Na Noelina Kimolo, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeushukuru Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa msaada wa vifaa tiba katika kitengo cha akina mama wajawazito na kitengo cha meno kwa lengo la kuboresha huduma katika Kituo cha Afya Makole vilivyotolewa na mfuko huo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka huu.
Shukrani hizo zimetolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dkt. Andrew Method kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika katika kituo hicho leo Juni 24, 2021.
Mganga Mkuu huyo alisema kuwa, vifaa hivyo vina umuhimu mkubwa katika kuendeleza na kuboresha huduma kwenye upande wa akina mama wajawazito hususani wale wanaohitaji upasuaji na meno.
“Tumepata dawa nyingi ambazo zinahitajika katika upasuaji pamoja na nyuzi, lakini pia tumepata dawa na vifaa ambavyo vitatusaidia katika upande wa meno” alisema Dkt. Method.
Dkt. Method alisema kituo hicho ni moja ya vituo ambavyo vinahudumia wananchi wengi hususan baada ya Serikali kuhamia Dodoma hivyo, wanaamini kwa msaada huo uliotolewa na PSSSF wananchi wengi watanufaika nao katika kupata matibabu.
Aidha, Dkt. Method alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mhe. Antony Mavunde kwa ushirikiano mkubwa anaouonesha kwa kuwatafuta wadau mbalimbali wa maendeleo wanaosaidia kuboresha huduma za afya katika Jiji la Dodoma.
Akikabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Hosea Kashimba alisema kuwa, taasisi anayoiongoza inatambua kazi kubwa inayofanywa na Kituo cha Afya Makole katika kutoa huduma za afya kwa wakazi wa Jiji wakiwemo watumishi wa mfuko huo.
“Kwa kuzingatia ujirani wetu huu, PSSSF imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa kituo hiki ikilenga kuboresha huduma zitolewazo kwani kama mjuavyo nia ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya na ili kuhakikisha tunaendeleza nia hiyo, katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu tunachangia vifaa tiba katika kitengo cha akina mama wajawazito na kitengo cha meno kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za tiba ya meno ikiwemo utengenezaji wa meno bandia” alisema Kashimba.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mhe. Antony Mavunde ambaye ndiye aliyepokea vifaa hivyo alitoa shukrani kwa (PSSSF) kwa niaba ya wananchi wa jimbo lake huku akitoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo wa PSSSF kusaidia huduma za afya katika Jiji la Dodoma.
“Katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu, tunatoa shukrani zetu kwa PSSSF kwa kutuletea msaada kwenye kituo hiki” alisema Mavunde kwa unyenyekevu. Aidha, Mhe. Mavunde alisema ushirikiano huo ni mzuri katika kutatua shida mbalimbali za wananchi pamoja na kuleta maendeleo katika katika Jiji la Dodoma na Taifa kwa ujumla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.