HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imewataadharisha wananchi kuepuka kununua viwanja kutoka kampuni inayojitambulisha kwa jina la Sanno Co. Ltd badala yake kufika katika ofisi za Halmashauri hiyo na kununua viwanja kwa mujibu wa taratibu.
Katika taarifa iliyotolewa kwa umma na Afisa Habari wa Halmashauri hiyo Dennis Gondwe leo jijini Dodoma, imesema kuwa kuna taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kampuni inayojitambulisha kwa jina la Sanno Co. LTD kuwa inauza viwanja katika eneo lililopo jirani na mji wa Serikali katika Kata ya Mtumba. “Wananchi wote wanatahadharishwa kuwa, taarifa hiyo ni ya uongo na kampuni tajwa haijapima wala haina viwanja ndani ya Jiji la Dodoma, hivyo muipuuze kwa sababu kumekuwa na wimbi la matapeli wanaowaibia wananchi fedha kwa kupitia uuzaji wa viwanja” amesema Gondwe.
Aidha, amewakumbusha wananchi kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ndiyo mamlaka pekee ya upangaji, upimaji, uuzaji, na umilikishaji wa viwanja katika Jiji la Dodoma. Mwananchi atakayenunua kiwanja jijini hapo nje ya utaratibu atakosa haki ya kumilikishwa kiwanja hicho kwa mujibu wa sheria, ameongeza.
Afisa Habari huyo amewashauri na kuwakumbusha wananchi wanaotaka kununua viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali kufika katika ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kufanya taratibu za kununua na kumilikishwa kiwanja kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.