HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imekamilisha zoezi la kutambua wazee katika Kata zote 41 za Jiji hilo, ambapo jumla ya wazee 19,543 wametambuliwa ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 inayolenga kuwaenzi kwa mchango wao katika Taifa kwenye nyanja mbalimbali ikiweno uchumi, siasa, kijamii na kiutamaduni.
Halmashuri hiyo pia tayari imewapatia vitambulisho wazee 10,290 ambavyo vitawatambulisha katika maeneo mbalimbali ya huduma ikiwemo kwenye vituo vya Afya, huku wengine 2,686 vitambulisho vyao vikiwa katika maandalizi.
Hayo yamebainishwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Jiji la Dodoma Rebeka Ndaki wakati akisoma taarifa ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwenye mkutano wa uzinduzi wa Baraza la Wazee Wilaya ya Dodoma jana katika ukumbi Halmashauri ya Jiji, mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi.
Alisema mpaka sasa Halmashauri ya Jiji kupitia Idara ya Afya imewafikia wazee katika Kata 33 kati ya 41 za Jiji hilo na kuwapiga picha wazee wapatao 12,979 sawa na asilimia 66.41 ya wazee wote waliotambuliwa ambapo tayari wazee 10,290 wameshapatiwa vitambulisho.
“Halmashauri ya Jiji katika kipindi cha kuanzia Mwezi Julai 2018 hadi Juni 2019 imetekeleza maelekezo ya Serikali ya kutoa huduma ya matatibu bure kwa wazee ambapo jumla ya wazee 4,551 walihudumiwa katika vituo vya huduma vya Jiji wakitumia vitambulisho vya wazee” ilisema sehemu ya taarifa ya Halmashauri hiyo.
Akizungumza na wazee hao kabla ya kuzindua rasmi Baraza hilo, Mkuu wa Wilaya Katambi alitoa wito kwa jamii nzima kuwajali na kuwaenzi wazee kwani wamefanya kazi kubwa katika ujenzi wa Taifa na kuweka mazingira rafiki kwa vijana wa sasa kuishi kwa amani na utulivu.
“Wazee ni tunu ya Taifa, juhudi zao za muda mrefu ndiyo zimetufikisha hapa kama Taifa kwahiyo ni lazima tuwaenzi kwa kila namna na mimi Ofisi yangu iko wazi wakati wote kwa ajili ya kuwahudumia na kusikiliza changamoto zao” alisema Katambi.
Mkuu wa Wilaya huyo aliitaka jamii hasa vijana kuacha dhana potofu kuwa wazee wamepitwa na wakati, kwani kwa uhalisia vijana ndiyo waliopitwa na wakati kwa kuwa wazee walikuwepo tangu zamani na sasa wapo tofauti na vijana ambao wa kizazi kipya.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.