Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kutekeleza agizo la kisheria la serikali la kutenga na kutoa asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo isiyo na riba ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Pongezi hizo zilitolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mwita Waitara alipofanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo kukagua shughuli za kikundi cha vijana kiitwacho Tujikomboe pamoja na miradi mingine ya maendeleo.
Waitara alisema kuwa Halmashauri ya jiji la Dodoma inafanya vizuri katika kutekeleza agizo la kisheria la Serikali la kutenga asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Alisema kuwa mikopo hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa makundi hayo na kuyawezesha kujikwamua kiuchumi.
Akiongea na vijana wa kikundi hicho, Naibu Waziri aliwataka kufanya kazi kwa juhudi na umakini mkubwa. “Serikali haiwezi kuajiri watu wote ndiyo maana inatengeneza mazingira na miundombinu rafiki ili kila mtu aweze kuzalisha na kuchangia ujenzi wa nchi” alisema Waitara. Vilevile, aliwataka wanakikundi hao kuwa waaminifu na kuhakikisha wanarejesha kwa wakati mkopo waliokopeshwa ili vijana wengine waweze kukopeshwa. Aliwakumbusha kuwa kukopa na kurejesha kwa uaminifu na kwa wakati kunawapa sifa ya kuendelea kukopesheka na Halmashauri. Aidha, alimuelekeza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kusimamia kwa karibu fedha hizo zinazotolewa kwa vikundi ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema kuwa takribani zaidi ya shilingi bilioni tatu zimetolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Alisema kuwa fedha hizo ni zaidi ya asilimia 110 kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Halmashauri ya jiji itaendelea kusimamia vikundi vyote vilivyokopeshwa ili viweze kufikia malengo yake na malengo mapana ya serikali, aliongeza Kunambi.
Kikundi cha vijana Tujikomboe kilianzishwa mwaka 2015 kna kusajiliwa mwaka 2018 kikiwa na vijana watano. Kikundi kimefanikiwa kukopeshwa mkopo wa shilingi milioni 10 na Halmashauri ya Jiji la Dodoma mwishoni mwa mwezi Mei, 2019 kwa ajili ya kukiwezesha kukuza mtaji wake na shughuli za maendeleo za kikundi hicho.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.