HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imekabidhi vifaa mbalimbali kwa vikundi vya ujasiliamali ikiwa ni pamoja na lori aina ya fuso lenye uwezo wa kubeba tani saba kwa ajili ya kubebea mchanga na matofali, kutoka asilimia kumi ya mapato ya ndani ambayo yanatakiwa kurejeshwa kama mkopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
Akikabidhi mikopo hiyo leo Februari 3, 2022, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mheshimiwa Jabir Shekimweri amesema kuwa mikopo hiyo ni kwa ajili ya shughuli za viwanda, Guta 1, Lori moja la kubebea tofari na mchanga aina ya fuso tani saba na mikopo kwa ajili ya biashasha ndogondogo, mikopo ya kilimo, mikopo ya mifugo na mikopo kwa ajili ya mama lishe na baba lishe.
Shekimweri alisema kuwa katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi 817,400,000 kwa vikundi 78 vilivyokabidhiwa hundi zao leo.
"Mikopo hii itumike katika kuwaletea maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja, jamii inayomzunguka pamoja na taifa kwa ujumla kwa kutimiza nia ya serikali ya kukuza uchumi wa mtu na uchumi wa watu" alieleza Shekimweri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru alisema kuwa, katika kutekeleza sera ya kutoa asilimia kumi katika makundi ya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu. Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kipindi cha mwaka wa fedha imetoa jumla ya mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 8.87.
"Vile vile taarifa inaonesha kwamba shilingi 3,981,070,933.62 tu ndizo zimerejeshwa, sawa na asilimia 44.9 ya kiasi kilichotolewa kwa mikopo ". Amesema Mafuru.
Mkurugenzi Mafuru amesema kuwa katika mikopo iliyotolewa leo kwa upande wa vikundi 46 vya wanawake, wamepata shilingi 395,000,000, vikundi 23 vya vijana wamepata shilingi 364,000,000 na vikundi 19 vya watu wenye ulemavu wamepata shilingi 58,400,000 na kufanya jumla ya vikundi 78 kupata jumla ya fedha kiasi cha shilingi 817,400,000.
Naye Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde amewataka wanavikundi wote wanaonufaika na mikopo hiyo kuitumia kwa lengo lililokusudiwa huku akiimwagia sifa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekeleza kwa kiwango kikubwa takwa hilo la kisera la kutoa asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa makundi hayo.
Akitoa ushuhuda katika hafla hiyo, mwenyekiti wa kikundi cha Ilumbo Group ambacho kilishanufaika na utaratibu huo Monica Masado alisema kikundi hicho kimekuwa wanufaika wakuu wa mikopo kutoka katika halmashuri ya Jiji la Dodoma.
Monica amesema kuwa mikopo hiyo ambayo inatolewa na halmashauri ya Jiji imeweza kuinua maisha ya watu pamoja familia zao.
Hata hivyo amewakumbusha wakopaji wanaokopa mikopo hiyo kuhakikisha wanakopa na kurejesha kwa wakati ili fedha hizo ziweze kutumika kukopesha vikundi vingine.
Naibu Meya wa Jiji la Dodoma Mheshimiwa Emmanuel Chibago amewataka wakopaji kufanya shughuli za maendeleo badala ya kukopa na kutumia fedha hizo kwa shughuli tofauti na makusudio ya kikundi jambo ambalo linaweza kusababisha kushindwa kufanya marejesho ili vikundi vingi zaidi viweze kukopeshwa na Halmashauri hiyo.
Mhe. Chibago amesema kuwa Baraza la Madiwani la Jiji la Dodoma limefanya wajibu wake katika kusimamia ukusanyaji na matumizi sahihi ya mapato ya Jiji. Mikopo inayotolewa ni ushahidi kuwa madiwani wamefanikiwa kutekeleza kile ambacho wananchi wa Jiji la Dodoma waliwachagua ili kwenda kukitekeleza kwa faida ya wananchi wao.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri akiongea na hadhara iliyohudhuria hafla ya utoaji mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu katika Jiji la Dodoma.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mafuru akitoa ufafanuzi wa utoaji wa mikopo na mikakati ya Jiji la Dodoma katika kutekeleza kwa ufanisi utoaji wa mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na wenye ulemavu.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana Asha Vuai akisoma taarifa ya utoaji mikopo kwa vikundi.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi kutoka Jiji la Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri (wa tatu kushoto) akikata utepe kuzindua vyombo mbalimbali vya usafiri vilivyotolewa kwa vikundi. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Naibu Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Mhe. Emmanuel Chibago (kushoto kwa mgeni rasmi), Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Mhe. Anthony Mavunde (wa tatu kushoto), Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma, Meja Mstaafu Johanick Lisasi (mwenye shati la kijani).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.