Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa jumla ya vibali vya ujenzi 7,133 katika kipindi cha miaka mitatu katika kudhibiti ujenzi holela.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aisha Masanja alipokuwa akiwasilisha mada juu ya uboreshaji wa makazi ndani ya Jiji la Dodoma katika maadhimisho ya siku ya makazi duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma.
Masanja alisema kuwa Halmashauri imekuwa ikipokea maombi ya vibali vya ujenzi kwa kasi kubwa tangu Halmashauri hiyo kutangazwa kuwa Jiji. “Katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2017 hadi Juni, 2020 jumla ya vibali vya ujenzi 7,133 vimetolewa” alisema Masanja. Vibali vya ujenzi hutolewa ndani ya siku saba kwa maombi ambayo hayana shida, aliongeza.
Akiongelea athari za uendelezaji ujenzi usiozingatia kanuni, taratibu na sheria za mipango miji, Afisa Mipango Miji huyo alisema kuwa unasababisha jiji kukua bila kufuata taratibu zilizopo. Alisema kuwa ukiukwaji wa taratibu hizo hupelekea ujenzi wa majengo yasiyo na mpangilio. Athari nyingine aliitaja kuwa ni kukosekana kwa maeneo ya huduma za kijamii na miundombinu muhimu, hivyo kufikika kwa shida wakati wa majanga.
Afisa huyo aliongeza athari nyingine ni kupata hasara pindi hatua stahiki za mipango miji zitakapochukuliwa kama ubomoaji ili kupisha miundombinu muhimu. “Ndugu washiriki, athari nyingine ni kukosekana kwa mvuto wa ujenzi” aliongeza Masanja.
Afisa Mipango Miji huyo alisema kuwa katika kufanikisha udhibiti ujenzi holela, Watendaji wa Kata na Mitaa wanawajibu wa kuhakikisha hakuna uvamizi kwenye maeneo ya wazi, hifadhi za barabara na maeneo ya taasisi. “Watendaji wanawajibu wa kuhakikisha wanapata nakala ya mabadiliko ya matumizi ya ardhi au mgawanyo wa kiwanja kwa wananchi watakaoweka mabango katika maeneo yao. Pia, wanawajibu wa kutoa taarifa Halmashauri kama kuna ujenzi wowote usiokuwa na kibali katika maeneo yao” alisema Masanja.
Watendaji Kata na Mitaa wanawajibu wa kukagua ujenzi unaofanyika katika maeneo yao kwa kuhakikisha kuwa wana vibali vya ujenzi. “Halmashauri ya Jiji tumeanzisha matumizi ya rangi ya kupaua au kupakwa katika mapaa ya majengo kwa kata zote 41 za jiji la Dodoma. Katika kutekeleza lengo hili, watendaji wanatakiwa kuhakikisha watu wanajenga na kuezeka kwa kufuata rangi za bati zilizopangwa katika Kata zao” alisisitiza Masanja.
Maadhimisho ya siku ya makazi duniani yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Nyumba bora kwa wote; kwa ukuaji bora wa miji”.
Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aisha Masanja alipokuwa akitoa mada uu ya uboreshaji wa makazi ndani ya Jiji la Dodoma kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Jijini Dodoma leo 05 Octoba, 2020.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.