HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.39 kutoka mapato yake ya ndani kutekeleza mipango na uimarishaji Elimu ya Sekondari kwa lengo la kuboresha miundombinu ya kujifunzia.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmshauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari baada ya kutembelea na kukagua miundombinu ya Shule za Sekondari katika jiji la Dodoma jana.
“Halmashauri ya Jiji imepeleka shilingi bilioni 1.39 kutekeleza miradi mbalimbali katika Elimu ya Sekondari kupitia mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2018/2019” alisema Kunambi.
Alisema Halmashauri hiyo ilikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 52, na kusababisha wanafunzi 2,610 waliofaulu kukosa madarasa.
“Ujenzi wa madarasa mapya 37 na ukarabati wa madarasa mengine utaliwezesha Jiji kuondoa tatizo la upungufu wa madarasa, na kuwawezesha wanafunzi wote waliofaulu kupata madarasa ya kutosha” alisema.
Akielezea sababu za upungufu huo, Mkurugenzi huyo alisema kuwa, umetokana na ongezeko la ufaulu mkubwa kufuatia juhudi za Serikali kutoa Elimu ya Msingi bila malipo.
“Tunamshukuru sana Rais wa Awamu ya Tano, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa Elimu bila malipo…ongezeko la ufaulu ni juhudi kubwa za Mhe. Rais na katika kuhakikisha tunaunga mkono juhudi hizo, sisi tumepeleka kiasi hicho cha Fedha kutoka mapato ya ndani kwenye sekta ya elimu.
Akiongelea ujenzi wa maabara za masomo ya Sayansi, Kunambi alisema ujenzi wa maabara 15 za masomo ya Sayansi zinakwenda kwa kasi.
“Maabara hizi lazima zijengwe kwa ubora unaoendana na hadhi ya Jiji la Dodoma na lengo ni kuhakikisha Shule zote zinakuwa na maabara za kisasa zenye vifaa ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo” aliongeza.
Kunambi alifanya ziara ya kutembelea na kukagua miundombinu ya ujenzi wa madarasa na maabara katika shule za sekondari Miyuji, Umonga na Dodoma, ambapo aliambatana na Mchumi na Ofisa Elimu wa Idara ya Sekondari.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.