HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imefanikiwa kukusanya shilingi 71,921,804,660 sawa na asilimia 107.1 na kwa mara nyingine kuvuka lengo la makusanyo ya ndani ya Halmashauri hiyo safari hii kwa asilimia 7.1.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za serikali kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2018/2019 katika mkutano wa mwaka wa Baraza la Madiwani lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Kunambi alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 bajeti ya makusanyo ya ndani ilikuwa shilingi 67,149,647,027. Halmashauri hiyo ilikusanya shilingi 71,921,804,660 sawa na asilimia 107.1 na kuvuka lengo la makusanyo ya mapato ya ndani kwa asilimia 7.1.
Akiongelea ongezeko la bajeti ya Halmashauri, alisema kuwa bajeti iliongezeka kutoka shilingi 20,798,303,295 mwaka wa fedha 2017/2018 hadi kufikia shilingi 67,149,647,027 mwaka wa fedha 2018/2019 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 69.02.
Kuhusu mapato halisi ya ndani, yameongezeka kutoka shilingi 25,058,290,451 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi kufikia shilingi 71,921,804,660 kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 65.15, aliongeza.
Akifafanua zaidi kuhusu bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019, Mkurugenzi huyo alisema kuwa Halmashauri ilikisia kukusanya na kupokea jumla ya shilingi 159,467,035,337 bila bakaa ya mwaka wa fedha 2017/2018. Fedha kutoka vyanzo vya ndani shilingi 67,149,647,027, ruzuku ya mishahara shilingi 44,599,110,165, ruzuku ya matumizi mengineyo shilingi 6,924,823,507 na ruzuku ya miradi ya maendeleo shilingi 40,793,454,638.
Katika mapato, alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/19 Halmashauri ilifanikiwa kupokea jumla ya shilingi 168,446,315,814. Kati ya fedha hizo, shilingi 71,921,804,660 ni vyanza vya ndani vya Halmashauri, shilingi 45,279,048,720 ni ruzuku ya mishahara, shilingi 2,478,129,023 ni ruzuku ya matumizi mengineyo na shilingi 48,767,333,411 ni ruzuku ya miradi ya maendeleo.
Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi kutoka kwa Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepata hati safi kwa miaka miwili mfululizo mwaka 2016/2017 na 2017/2018.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.