HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeongeza masaa ya mawili kila siku kwa shule za sekondari ili kufidia muda uliopotea katika mapumziko ya ugonjwa wa Covid-19 kwa lengo la kutoathiri muhtasari wa elimu na kuwapatia wanafunzi elimu inayostahili kwa mujibu wa ratiba.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokuwa akiongelea maadalizi ya kufungua shule za sekondari katika Halmashauri hiyo.
Mwalimu Rweyemamu alisema kuwa sehemu kubwa ya muda wa masomo imepotea katika mapumziko ya ugonjwa wa Covid-19.
“Muda uliopotea lazima tuufidie, hakuna namna. Halmashauri ya Jiji la Dodoma tumefanya vikao na wakuu wa shule na Maafisa Elimu Kata na tumeamua kwa pamoja kuongeza masaa mawili kila siku ya kufundisha wanafunzi. Hivyo, ratiba zetu za vipindi zinakwenda kurekebishwa. Kwa maana hiyo badala ya wanafunzi wa sekondari kutoka saa 9 alasiri watakuwa wanatoka saa 11 jioni.
Alisema kuwa pamoja na kuongeza masaa mawili kila siku, nayo hayatoshi. Hivyo, siku ya Jumamosi wanafunzi watakuwa na ratiba shuleni. “Halmashauri ya Jiji tunatarajia kwamba tukifanya haya, zile siku za mwanafunzi kupata elimu shuleni zitatimia” aliongeza Mwalimu Rweyemamu.
Aidha, aliwataka walimu na wazazi kuzingatia mabadiliko ya ratiba hiyo ili kwenda sambamba na muhtasari wa elimu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Afisa Elimu huyo alisema kuwa wamekubaliana shule zote zipange ratiba ya mikutano na wazazi wiki ya kwanza baada ya shule kufunguliwa ili kuweka utaratibu wa chakula cha mchana kwa wanafunzi. “Ukishaongeza masaa ya kukaa shuleni kwa mwanafunzi, lazima uangalie suala la chakula kwa wanafunzi hao. Wito wangu kwa wazazi, tukiitwa shuleni twende tuangalie jinsi watoto wetu watakavyopata chakula shuleni. Haitakuwa na maana kwa mwalimu kumfundisha mwanafunzi mwenye njaa, hataelewa. Tunatamani wanafunzi wetu wasome wakiwa wameshiba” alisisitiza Mwalimu Rweyemamu.
Akiongelea tahadhari ya kuenea kwa virusi vya Corona baada ya shule hizo kufunguliwa, alisema kuwa maelekezo na miongozo ya kukabiliana na virusi hivyo imetolewa kwa mujibu wa wizara ya afya ili wote wawe na uelewa wa pamoja.
Itakumbukwa kuwa agizo la kufunguliwa shule zote nchini lilitolewa na Rais, Dkt. John Magufuli alipokuwa akilihutubia kwa mara ya mwisho Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukumbi wa Bunge tarehe 16 Juni, 2020 jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.