MFUKO wa uhifadhi mazingira na wanyama pori duniani (WWF) kwa kushirikiana na Vodacom Foundation Tanzania wakiwa sambamba na Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamefanya usafi katika soko la Chang’ombe Jijini Dodoma mapema leo Novemba 26, 2019 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi rasmi wa mradi wa usafi kwa kuzuia takangumu na kukijanisha Dodoma.
Zoezi hilo limefanyika ili kuunga mkono kauli ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania idara ya mazingira ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani kwa kufanya usafi na kupanda miti.
Mhandisi wa mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Juma Limbe amewashukuru wadau wa mazingira na kuwaomba watu wengine wajitokeze kuhakikisha nchi yetu inakuwa usafi kwa kupanda miti na kuhifadhi taka vizuri hasa zile ngumu na za plastiki.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri Jiji la Dodoma, Afisa mazingira wa Jiji hilo Ally Mfinanga alisema kuwa, mradi huo ni jitihada za kuifanya Makao Makuu kuwa katika hadhi yake na kutokomeza ukame kabisa ili kuepusha majanga yanayotokana na uchafu na kwamba yeyote atakaebainika kuharibu mazingira atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Hizi ni hatua za kwanza za mradi endelevu wa usafi wa kuzuia plastiki na kukijanisha Dodoma ambao unalenga kupanda miti na kufanya usafi katika sehemu za taasisi kama shule, masoko, vyuo, pembezoni mwa barabara na sehemu zingine” alisema Mratibu miradi wa mfuko wa uhifadhi mazingira na wanyama pori (WWF) Savinus Kessy.
Kwa upande wake meneja ruzuku na mawasiliano kutoka kampuni ya Mawasiliano ya simu za mkononi ya Vodacom Foundation Tanzania Sandra Osward alisema kuwa, mradi huo utadumu kwa miaka mitatu ambapo katika awamu hii ya kwanza umeanza Jijini Dodoma tangu mwezi Agosti na utamalizika mwezi Machi mwaka 2020, na baadae utatekelezwa katika mikoa mingine ili kuendelea kuhamasisha wananchi kufanya usafi.
Katika zoezi hilo, wafanyabiashara walijitokeza kwa wingi kuungana na wadau hao kufanya usafi , ambapo mmoja wa wafanya biashara hao Zainabu Moses alisema anatamani sana zoezi hilo liwe linafanyika mara kwa mara ili soko liwe safi wakati wote.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.