Na Josephina Kayugwa, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetoa fursa kwa kuwakaribisha wawekezaji na Halmashauri nyingine kuwekeza katika ardhi ya Dodoma kwa lengo la kujiongezea mapato na kukuza uchumi, kwa sababu Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina vitega uchumi na sehemu nyingi ambazo zinaongeza mapato na kuleta maendeleo.
Hayo yalisemwa leo na Mchumi wa Jiji, Amani Ng’oma, alipokuwa katika ziara iliyofanywa na madiwani kutoka Manispaa ya Temeke ambao walifanya ziara kwa nia ya kujifunza na kuona miradi mbalimbali inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia mapato ya ndani na Serikali kuu.
“Jiji la Dodoma lina ardhi ambayo inaweza kuruhusu hata wawekezaji kutoka Halmashauri nyingine kuwekeza na kufanya miradi mikubwa ya kimaendeleo, miradi ambayo itawafanya kuongeza mapato kwao na kwa Jiji la Dodoma.
Uwekezaji unaofanywa na Jiji la Dodoma ni mkubwa na unahamasa kwa wengine ambao wanakuja kujifunza kwetu kwa sababu miradi ambayo inatekelezwa asilimia kubwa inatumia mapato ya ndani kwa hiyo hata Wilaya nyingine zinaruhusiwa kuja kufanya uwekezaji hapa Dodoma ili tusaidiane kuinua uchumi wetu wa Nchi,” alisema Ng’oma.
Kwa upande wake Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Anuary Peter amesema malengo ya ziara katika Jiji la Dodoma yamekamilika kwa sababu wamepata kujifunza mengi na kuona jinsi gani Jiji la Dodoma limeweza kufanikisha miradi yenye tija ambayo inawaongezea mapato.
“Miradi yote tuliyoitembelea ni mizuri na imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa nasi tumejifunza mengi na mazuri kwa hiyo tutaenda kuyafanyia kazi yote tuliyojifunza na kuyapata ili tuweze kuwa kama Dodoma kimaendeleo.
Nitoe pongezi kwa Uongozi wa Jiji la Dodoma kwa kufanya utekelezaji mkubwa wa miradi, kiukweli mimi nimejifunza mengi ikiwemo mradi wa Soko la wazi la Machinga kwa sababu mpangilio na utaratibu uliofanyika katika kuwasajili na kuwapanga wafanyabiashara ni mzuri,” alisema Peter.
Miradi yote inayotekelezwa na Halmashauuri ya Jiji la Dodoma inatumia mapato ya ndani, miradi hiyo ni kama Soko la wazi la Machinga, “Dodoma City Hotel”, Kituo cha Maegesho ya Malori - Nala na Jengo la kitega uchumi - Mtumba, miradi hii itasaidia katika kuinua uchumi wa Jiji la Dodoma na kuzalisha ajira kwa wakazi wake.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.