MKUU wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoa semina elekezi na kuwapatia mafunzo kwa vitendo, vijana watakao wapa ajira ya muda kwenye mradi wa utekelezaji wa uwekaji wa anwani za makazi utakaofanyika katika mitaa 222 ya kata 41 za Jiji hilo ili waweze kufanya kazi hiyo kwa uadilifu, uaminifu na uzalendo.
Shekimweri ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kata ya Ipagala mtaa wa Swaswa Ng’ambo Jiji la Dodoma kwenye uzinduzi wa utekelezaji wa mfumo wa uwekaji wa anwani za makazi uliofanyika kwa ngazi ya wilaya katika eneo hilo.
Alisema halmashauri ya jiji inatakiwa kutoa semina elekezi pamoja na mafunzo kwa ya vitendo kwenye maeneo ya mradi huo wa uwekaji wa anwani na makazi ili vijana watakaoajiriwa waweze kujifunza na kuifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa, uaminifu na uzalendo zaidi.
Pia, Mkuu huyo wa wilaya ametoa angalizo kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuwataka kuhakikisha vijana watakaoajiriwa kwa ajili ya kazi hiyo muda ya utekelezaji wa uwekaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi miongoni mwao wawe wanaotoka eneo wanaloishi.
“Mimi kama mkuu wa wilaya ya Dodoma nitashangaa sana ikiwa halmashauri itaajiri vijana wa kutoka nje ya mikoa na kata na mitaa husika, hivyo nitoe angalizo kuhakikisha watakaowaajiri wawe wanatoka maeneo wanayoishi na siyo vinginevyo” alisisitiza.
Katika hatua nyingine Shekimweri ametoa wito kwa vijana watakaopata ajira hiyo ya muda kuhakikisha wanaifanya kazi hiyo kwa uzalendo uadilifu mkubwa na uaminifu ili waweze kukamilisha kwa zoezi hilo kwa wakati.
Naye Mratibu wa mfumo wa uwekaji za anwani za makazi Jiji la Dodoma Joseph Nkuba alisema kuwa utekelezaji wa mradi huu mkubwa ni muhimu sana wa mfumo wa anwani za makazi kwa kuwa ni maelekezo na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba una faida nyingi ikiwemo kurahisisha utoaji huduma pamoja na masuala ya usalama wa wananchi.
“Halmashauri hii ya Jiji la Dodoma mradi ulianza rasmi Desemba 15, 2021 kwa kutambua mipaka ya mitaa ya kiutawala ambapo mpaka sasa tumeitambua mipaka 153 kati ya mitaa 222 na mitaa 69 bado haijatambuliwa mipaka yake na zoezi linalofuatia ni kutambua namba za nyumba na kuchukua taarifa za wakazi na kuzisajili kwenye mfumo” alisema.
Nkuba akizungumza kwenye uzinduzi huo alibainisha kuwa, zoezi hili siyo jipya bali ni mwendelezo kwa kuwa tayari mitaa nane ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilishawekewa anwani za makazi, na kwamba tofauti ni kuwa kwa sasa itawekwa kwenye mfumo maalum wa kutumia simu janja.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.