HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetakiwa kujipanga katika uendeshaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa ili isimamiwe vizuri pasipo kuathiri jukumu lake la msingi la utoaji huduma kwa wananchi.
Kauli hiyo alitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alipofanya ziara ya kawaida ya kutembelea na kukagua miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma jana.
Dkt. Mahenge alisema “nimejiridhisha na utekelezaji wa miradi yote mitatu inaenda vizuri sana. Mkandarasi Mohammedi Builders unafanya kazi nzuri. Pongezi kwa Mkurugenzi wa Jiji na Mkuu wa Wilaya kwa kazi nzuri ya usimamizi”. Aliongeza kuwa uwekezaji huo mkubwa unatarajiwa kukamilisha tarehe 31 Disemba, 2019, na kuitaka Halmashauri kuanza kujipanga itakavyosimamia miradi hiyo na kuifanya kuwa endelevu.
Mkuu wa Mkoa alishauri kuwa baada ya taratibu za uendeshaji wa miradi hiyo kukamilika, mwezi Novemba, 2019 miradi hiyo ianze kutangazwa ili wananchi wa Dodoma na maeneo mengine waanze maandalizi ya uwekezaji katika miradi hiyo. Vilevile, alivikaribisha vikundi mbalimbali, vyuo, shule na wajasiriamali kutembelea maeneo hayo kujionea uwekezaji huo mkubwa na fursa za wao kuwa sehemu ya uwekezaji.
Akiongelea ujenzi unaofanywa na kampuni ya Mohammedi Builders, mkuu wa mkoa alisema anaridhishwa na kazi inayofanywa na mkandarasi huyo. “Mkandarasi Mohammedi Builders unafanya kazi nzuri. Kujenga miradi mitatu kwa pamoja na yote inakwenda vizuri siyo jambo dogo. Nimeridhishwa miradi yote mitatu inakwenda vizuri” alisema Dkt. Mahenge.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi aliitaja ziara ya Mkuu wa Mkoa kuwa ni kujionea kazi inayofanywa na Rais, Dkt. John Magufuli jijini Dodoma. “Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali jijini Dodoma. Miradi yote ina hadhi ya Makao Makuu na itakuwa na faida kubwa kwa wakazi wa Dodoma” alisema Kunambi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alifanya ziara ya kawaida kutembelea na kukagua miradi ya kimkakati ya uboreshaji wa mandhari ya eneo la kupumzikia (Recreational park) katika eneo la Chinangali, ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi na soko kuu katika eneo la Nzuguni inayotekelezwa na Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.