HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa ujenzi na uendeshaji wa jalala la kisasa 'dampo' la Chidaya katika jitihada zake za kuhakikisha usafi wa Jiji unaimarishwa na kulinda afya za wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi wa timu ya wataalam kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza Mhandisi Henry Mbaga walipotembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujifunza juu ya ujenzi na uendeshaji wa jalala la kisasa Chidaya.
Mbaga alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefanikiwa katika ujenzi na uendeshaji wa jalala la kisasa Chidaya. “Timu ya wataalam kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza imetembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya kujifunza jinsi wenzetu walivyofanikiwa katika ujenzi na uendeshaji wa jalala la kisasa. Tunataka kujifunza pia kupitia changamoto ambazo wenzetu wa Dodoma wanakutana nazo na kufanikiwa katika uendeshaji na kubadilishana uzoefu ili tunapoanza kujenga tujenge kwa ufanisi” alisema Mhandisi Mbaga.
Mhandisi huyo alisema kuwa timu yake imejifunza kuwa ushirikishaji wa wadau wanaotekeleza usafi wa mazingira ni jambo la msingi. “Ushirikishaji wa wadau wa usafi wa mazingira ni muhimu, tumeona kuwa mdau anatekeleza majukumu yake ipasavyo na kuwa Halmashauri ndiyo inaratibu. Lakini pia kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wakati ili kutokwamisha shughuli za usafi” alisema Mhandisi Mbaga. Vilevile, wamejifunza kuwa uangalizi na matengenezo ya mitambo kwa muda muafaka kunaliwezesha dampo kudumu na kufanya kazi au kutumika kwa muda mrefu.
Katika kutembelea jalala la Chidaya, angalizo lilikuwa wakati wa ujenzi mabomba ya kutolea maji machafu yalindwe ili yaweze kupita vizuri na kuepuka magari kutitia wakati wa mvua. Utaratibu huo utasaidia kuzuia maji yatokanayo na taka kuzuiwa kutokwenda kwenye maeneo husika, aliongeza.
Kwa upande wake, msimamizi wa jalala la kisasa la Chidaya, Godfrey Ngowi alisema kuwa mafanikio katika uendeshaji wa jalala hilo yanatokana na ushirikiano baina ya idara mbalimbali za Halmashauri na wadau. “Ushirikiano huu umekuwa ukiwezesha mahitaji kama mafuta, vilainishi vya mitambo, matengenezo ya mitambo kupatikana kwa wakati” alisema Ngowi.
Mtambo wa kusambaza taka ngumu ukifanya kazi katika dampo la kisasa la Chidaya
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.