Na Noelina Kimolo, DODOMA
MKUU wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsi na Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Sharifa Nabalang’anya, amewataka wajasiliamali wa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu kufanya marejesho ya fedha wanazokopeshwa na Halmashauri hiyo kwa wakati ili vikundi vingi zaidi viendelee kunufaika kupitia uwezeshwaji huo.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa hafla ya kukabidhi mkopo wa shilingi milioni 953 uliotolewa na Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na benki ya NMB iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, ambapo jumla ya vikundi 86 vimepokea mkopo huo kwa mchanganuo wa 54 wanawake, 28 vijana na 4 ni watu wenye ulemavu.
“Kuna vikundi vingi vinasubiri fedha hivyo mnatakiwa kufanya marejesho kwa muda sahihi ili muweze kuwasaidia na vikundi vingine kupata fedha hizo’’ alisema Nabalang’anya.
Mkuu huyo wa idara alisema kuwa, vikundi vinavyokopeshwa vihakikishe wanafanya kazi kwa bidii na kupata faida ambayo itawasaidia katika kufanya marejesho.
Kwa upande wake, mwanachama wa kikundi cha Faraja ya Kweli kutoka Kata ya Kizota Luciana Cyprias alisema kuwa wamejipanga kutumia vyema fedha hizo kwa kuendeleza biashara ili waweze kujinufaisha kiuchumi.
Mmoja wa wanakikundi walionufaika na mkopo huo kutoka kikundi cha vijana cha UAMUSHO Emmanuel Mjilima alisema kuna umuhimu wa kupatiwa semina sababu wanavikundi wengi hawana elimu ya matumizi ya fedha hususan linapokuja suala la mikopo katika kuhakikisha faida inatengenezwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.