HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma ikishirikiana na wananchi na wadau wa maendeleo wa Kata ya Kizota wanaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya katika hiyo ili kupeleka karibu zaidi huduma za matibabu ya afya kwa wananchi.
Mradi wa Kituo cha Afya Kizota uliibuliwa mwaka 2019 na kuanza kutekelezwa mwaka 2020. Kutokana na kutokuwa na fedha ya kutosha wakati utekelezaji unaanza, ambapo kulikuwa na kiasi cha shilingi milioni 70 tu (fedha za wananchi zilizotokana na mradi D-Center ya Mnada Mpya) Mhandisi wa Jiji alishauri yaanze kujengwa majengo matatu tu ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la huduma za mama na mtoto (RCH) na jengo la utawala. Tayari kiasi cha shilingi 78,814,180 fedha za wananchi wa kata ya Kizota na wadau mbalimbali wa maendeleo zimeshatumika katika ujenzi huo.
Aidha, mwishoni mwa mwezi wa Machi, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa kiasi cha shilingi 167,996,242 ambazo zimesaidia kuanza kwa ujenzi wa jengo la maabara. Majengo yote yanatarajiwa kukamilika mwezi wa saba na huduma zitaanza kutolewa kwa wananchi mara moja.
Aidha, inakadiriwa hadi kukamilika kwa majengo yote ya kituo, itagharimu kiasi cha shilingi milioni 600 kinahitajika.
Naye diwani wa kata ya Kizota, Mheshimiwa Jamal Ngallya akihojiwa na mwandishi wetu amesema “Mchakato wa kujenga kituo hicho cha afya ulianza kwa kutumia fedha za nguvu ya wananchi ambazo tulizipata kupitia malipo ya vibanda vya maeneo ya kufanyia biashara katika Kituo cha Daladala Mnada-mpya”
Mhe. Jamal amesema kuwa katika malengo ya baadae ni wanatarajia kukifanya kituo hicho kuwa na huduma zote za kulaza wagonjwa, kufanya upasuaji, n.k.
Uwepo wa kituo hicho cha afya utahudumia na kata za jirani na kupunguza msongamano katika hospitali kuu ya rufaa ya mkoa na Kituo cha Afya Makole.
“kwa wananchi wa Kata ya Kizota naomba kutoa shukrani kwa kuweza kuonyesha ushirikiano katika masuala ya kimaendeleo katika Kata yetu, hii inakuja baada ya wananchi hao kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa kituo cha afya cha Kata hiyo” amesema Diwani huyo wa Kata ya Kizota.
Diwani wa Kata ya Kizota Mheshimiwa Jamal Ngallya alipokuwa akiongea na mwandishi wa tovuti hii kuhusu ujenzi wa Kituo cha Afya Kizota.
Baadhi ya picha za majengo ya kituo cha Afya cha Kizota kinachoendelea kujengwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.