WANANCHI wa mtaa wa Mahomanyika jijini Dodoma wametakiwa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (improved Community Health Fund - iCHF) ili waweze kutibiwa bure mwaka mzima.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya alipokuwa akihamasisha wananchi wa mtaa wa Mahomanyika, kata ya Nzuguni jijini hapa katika uzinduzi wa kampeni ya uhamasishaji mkubwa wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii Ulioboreshwa uliofanyika katika ofisi ya mtaa huo.
Nabalang’anya alisema kuwa ugonjwa haupigi hodi, hivyo wananchi wanatakiwa kujiandaa kukabiliana na ugonjwa kwa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii Ulioboreshwa. “Ndugu zangu, CHF iliyoboreshwa ni muhimu. Mheshimiwa diwani, napenda kuonesha masikitiko yangu kwa idadi ndogo ya wananchi waliojiunga na CHF” alisema Nabalang’anya kwa masikitiko.
“Shukrani kwa Rais, Dkt. John Magufuli kwa kuendelea kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya kila mwaka. Haya ni mapenzi makubwa ya Rais wetu kwa wananchi. Tumuunge mkono anatuhurumia wananchi. Ombi langu tujiunge na mfuko wa bima ya afya ili tutibiwe mwaka mzima” alisema Nyabalang’anya. Katika kuonesha nia njema ya serikali kwa wananchi wake, kaya moja ikichangia shilingi 30,000 watu sita katika kaya hiyo wanahudumiwa mwaka mzima na serikali inaongezea shilingi 30,000 aliongeza.
Awali mratibu wa CHF katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Patrick Sebyiga alisema kuwa lengo la maboresho ya CHF ni kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanajiunga na mfuko huo ambao utawasaidia kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
Mratibu huyo alisema kuwa dhumuni la kuboresha CHF ni kutenganisha watoa huduma za tiba na usimamizi wa bima, kuweka mfumo wa bima, kuongeza idadi ya wananchama, kutoa mfumo wa utambulisho utakaowezesha huduma kupatikana kwa mwanachama akiwa sehemu yeyote katika Mkoa wa Dodoma.
CHF iliyoboreshwa imebuniwa na wataalam wa mradi wa HPSS- Tuimarishe afya ikiwa imetumia uzoefu wa mifuko ya bima ya afya ya jamii kutoka India pamoja na matokeo ya tafiti zilizofanywa ndani na nje ya nchi.
Wananchi walioshiriki kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiunga na CHF iliyoboreshwa wakisikiliza kwa makini, viongozi wakiongea faida za kujiunga na CHF iliyoboreshwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.