HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeingiza viwanja 31 vya kimkakati sokoni kwa njia ya mnada ili kuweka uwazi katika zoezi la uuzaji viwanja hivyo na kuepuka mianya ya rushwa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Uhusiano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo muda mfupi kabla ya kuanza zoezi la uuzaji viwanja kwa njia ya mnada katika eneo la wazi la Manispaa ya zamani jijini hapa.
Fungo alisema “viwanja vinavyouzwa leo vipo 31, ukitaka kuviuza kwa utaratibu wa kawaida utaleta taharuki na mtafaruku mkubwa katika jamii”. Viwanja vyote vitakavyouzwa hapa vipo eneo la Nzuguni, ambalo ni eneo la kimkakati lenye mvuto wa kibiashara katika kitovu cha jiji la Dodoma, aliongeza.
Alisema kuwa uuzaji wa viwanja hivyo kwa njia ya mnada unaongeza uwazi na uwajibikaji kwa zoezi hilo. “Hapa hakuna mwanya wa rushwa katika zoezi hili. Nikuhakikishie hakuna mtu aliyekuja hapa akijua bei ya kianzio kwa kila kiwanja. Uzuri wa mnada, mtu anajipangia bei mwenyewe” alisisitiza Fungo. Zoezi hili litaondoa malalamiko ya kupendelea mtu au makundi katika jamii. Kupitia mnada huu, Halmashauri nayo itapata mapato yake kwa njia ya uwazi, alisisitiza Fungo.
Mshiriki katika mnada huo aliyejitambulisha kwa jina na Yusta Mushi, kutoka mkoani Arusha alipongeza uamuzi wa kuuza viwanja hivyo kwa njia ya mnada. “Niwashauri tu wasimamizi wa zoezi hili kuwa wakati mwingine waongeze wigo wa matangazo kwa muda wa kutosha kwenye vyombo vya habari ili watu wengi wapate fursa na muda wa kushiriki katika mnada kama huu. Mimi nimekuja jana jioni hivyo kuchelewa zoezi la kwenda kutembelea maeneo ya viwanja vinavyouzwa” alisema Mushi.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeingiza sokoni viwanja 31 vya matumizi ya taasisi (1), kituo cha mafuta (1), hoteli (20), maduka makubwa (2), na biashara (7) kwa ajili ya mnada ambavyo vimenadiwa na watu wenye maadili yasiyo na shaka katika jamii. Viwanja hivyo vipo eneo la Nzuguni unapojengwa uwanja wa Taifa, stendi kuu ya kisasa ya mabasi na soko kuu la kisasa. Pia vipo umbali wa Kilomita 7 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma na Kilomita 10 kutoka Mji wa Serikali - Mtumba.
Aidha, viwanja hivi vipo karibu na eneo la viwanja vya uwekezaji Njedengwa, na jirani na eneo ambalo litajengwa stesheni ya treni. Pia eneo hili lipo mkabala na uwanja wa sasa wa maonesho ya Kilimo na Mifugo maarufu uwanja wa Nanenane.
Maafisa wa Jiji la Dodoma walioendesha mnada wa uuzaji wa viwanja, pichani ni Alfred Mlowe - Mweka Hazina wa Jiji (kulia), Joseph Fungo - Afisa TEHAMA na Uhusiano wa Jiji (kushoto), Mtalemwa - Afisa Ardhi (wa pili kutoka kushoto) na Aisha Masanja - Afisa Mipango miji.
Chini: Baadhi ya wananchi walioshiriki katika mnada wa uuzaji viwanja 31 vinavyozunguka Soko kuu jipya na Stendi Kuu mpya eneo la Nzuguni Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.