MKUU wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo (pichani) ameweka jiwe la msingi katika mradi ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika kikosi cha 837 Chita JKT wilayani Kilombero, mkoani Morogoro ukitarajiwa kufanikisha uhakika wa chakula kwa vikosi vya jeshi hilo na taifa kwa jumla.
Lengo la ujenzi wa skimu hiyo ni kuwa na kilimo cha mpunga chenye tija kwa kulima ekari 24,000 kwa misimu miwili ya mwaka ifikapo mwaka 2025. Kwa sasa kikosi hicho kinalima ekari 1,000 kwa mwaka.
Jenerali Mabeyo pia aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mpunga na kuzindua msimu mpya wa kilimo huku akitaka JKT kuzalisha kwa tija kuondoa hali ya kutegemea chakula cha msaada nchi inapokuwa na upungufu.
Alisema mkakati wa kilimo unaendelea kutekelezwa na JKT ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya kutaka kuzalisha kwa tija na kuwa na uhakika wa chakula salama na kutekeleza uchumi wa viwanda.
“Tulizoea tukiwa na njaa tunaagiza chakula kutoka nje, tulizoea kuwatumia wafanyabiasha kutuletea chakula lakini vilevile tulizoea wakati wa njaa kupata chakula cha msaada, nadhani tunahitaji sasa kufika mwisho.
“Na sisi tunataka tuwe sehemu ya kutoa chakula kwa wanaohitaji ndani na nje ya nchi, kwa eneo hili la Chita hilo linawezekana kwa sababu ya kutekeleza kilimo mkakati,” alisema.
Alisema anaamini uwekaji jiwe la msingi katika ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ni kiashiria cha uzalishaji wenye tija kwa historia ya kilimo cha umwagiliaji ndani ya JKT.
Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya skimu ya umwagiliaji unatarajiwa kukamilika Juni mwakani na itakuwa ikifanya kazi asilimia 100. “Ni mapinduzi makubwa ndani ya JKT na ni imani mradi utakamilika kama ulivyopangwa,” alisema.
Alisema hadi sasa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi inachangia kwa asilimia 65 ya malighafi ya viwandani nchini hivyo uwezeshaji huo mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji, utaongeza malighafi na kupunguza fedha za kigeni zinazotumika kununulia malighafi nje ya nchi Jenerali Mabeyo alitoa Sh milioni 200 kusaidia kukamilisha miundombinu ya skimu ya umwagiliaji na kusisitiza kilimo kitakapoanza kisisimame.
Wakati huo huo aliwataka vijana wa kujitolea kufanya kazi kwa weledi bila kukata tamaa kwani manufaa makubwa yatapatikana kwao. Alitaka JKT kuhakikisha inaangalia uwezekano wa kuongeza wigo wa mazao hususani yanayotoa mafuta kama vile alizeti.
“ Ukilinganisha uzalishaji wa mafuta ya kupikia na mahitaji yetu tuna upungufu wa tani 220,000 hadi tani 340,000 na mwaka 2019 /2020 nchi yetu imetumia kiasi cha Sh bilioni 413 kwa ajili ya kuagiza mafuta,” alisema.
Alisisitiza: “Ni wajibu wetu sasa kuigeuza kuwa fursa kwa kuwekeza katika kilimo cha mazao yanayozalisha mafuta ya kula ili kiasi cha fedha Sh bilioni 413 kinachotumika kuagiza mafuta nje ya nchi kibaki JKT
Chanzo:HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.