Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amelivunja Jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji.
Rais, Dkt. Magufuli amefanya maamuzi hayo leo tarehe 24 Februari, 2021 kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo.
Waziri Jafo alisema kuwa, kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 84 cha Sheria ya Serikali za Mitaa, sura ya 288, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia tarehe 24 Februari, 2021.
“Kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 5 (1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za miji) sura ya 288, Rais, Dkt. John Magufuli ameipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam” alisema Waziri Jafo.
Waziri Jafo alisema kuwa taratibu nyingine za kisheria zitakamilishwa ikiwa ni pamoja na kuhamisha shughuli za iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo imevunjwa kwenye Halmashauri mpya ya Jiji la Dar es salaam na kuwapangia vituo vipya vya kazi watumishi wa halmashauri iliyovunjwa.
Aidha, mgawanyo wa mali na madeni ya iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo imevunjwa utafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za miji) sura ya 288 na Sheria nyingine zinazohusika.
Leo wakati Rais, Dkt. Magufuli akizindua daraja la juu la Kijazi, lililopo Ubungo, Dar es Salaam alisema kuwa anakusudia kulivunja Jiji hilo ili gharama zilizokuwa zinatumika kuendesha halmashauri hiyo zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo.
“Nategemea kufanya mabadiliko kidogo, mabadiliko haya ya kuwa na manispaa ambazo zinawakilisha maeneo halafu unakuwa na jiji ambalo linakaa halina maeneo yoyote, natarajia Jiji la Dar es Salaam kulivunja, nawaambia hapa ili tutengeneze Jiji la eneo fulani” alisema.
“…lakini kuwa na madiwani wanakaa juu, wanachangiwa hela na hawana miradi ya maendeleo, wanakula posho na hawakuchaguliwa na watu. Hili nitalikataza. Wale wanaojiandaa kuwa mameya wa Dar es Salaam na wanakaa hawana maeneo, wajue hilo limekwisha” alisema Rais, Dkt. Magufuli.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.