RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Magufuli leo tarehe 09 Novemba, 2020 amemuapisha Profesa Adelardus Lubango Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Hafla ya kuapishwa kwake imefanyika Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suhulu Hassan, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Ibrahim Hamis Juma, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na viongozi wengine mbalimbali.
Akizungumza baada ya kumuapisha Mhe. Rais Magufuli amesema Watanzania wana matumaini makubwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wanataka kuona Serikali yao inapata uwakilishi mzuri katika masuala ya kisheria , hivyo amemtaka kuhakikisha anasimamia vizuri kesi za Serikali na kuzitetea kwa uharaka mali za Serikali.
"Watanzania hawapendi kuona Serikali yao inashindwa katika kesi, kachape kazi, kawatetee Watanzania hasa wanyonge, katetee mali za Serikali na kwa haraka. Umefanya kazi nzuri katika kipindi chako cha kwanza, nataka ukafanya kazi vizuri zaidi, ukajipange sawasawa, ndio maana nakupongeza lakini wakati huo huo nakupa pole kwa majukumu haya" amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewatoa hofu viongozi wateule wote ambao wamekuwa na hofu ya kuondolewa ama kubadilishwa katika nafasi walizonazo baada ya yeye kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili, akisema hatarajii kufanya mabadiliko ya viongozi hao labda kwa wale watakaokuwa wanastaafu ama kutofanya vizuri katika majukumu yao.
"Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi, Viongozi wa Taasisi na Idara za Serikali na wengine wote chapeni kazi, simuondoi mtu kwenye nafasi yake labda aharibu yeye mwenyewe au astaafu" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Chanzo: Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU (instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.