Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 24 Novemba, 2019 amepokea kiasi cha shilingi Trilioni 1.05 zinazotokana na gawio na michango kutoka taasisi, mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa.
Hafla ya kupokea gawio na michango hiyo imefanyika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mabalozi, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC), viongozi wa Dini na viongozi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge.
Katika taarifa yake Msajili wa Hazina Bw. Athuman Mbuttuka amesema fedha za gawio na michango iliyowasilishwa leo kwa Mhe. Rais Magufuli ni ya mwaka wa fedha wa 2018/19 na imetoka katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni 79 kati ya taasisi, mashirika ya umma na kampuni zote 266 ambazo Serikali imewekeza mitaji, na kwamba kiasi hicho kimeongezeka kutoka shilingi Bilioni 161.04 zilizokusanywa katika mwaka 2014/15.
Bw. Mbuttuka amebainisha kuwa mafanikio ya kuongezeka kwa makusanyo hayo yametokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kuhakikisha taasisi, mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa zinaendeshwa kwa tija na kuzalisha gawio, ambapo idadi ya taasisi, mashirika ya umma na kampuni zinazotoa gawio na michango zimeongezeka kutoka 24 mwaka 2014/15 hadi kufikia 79 mwaka 2018/19.
Amebainisha kuwa maelekezo ya Mhe. Rais Magufuli pia yamesaidia kuongeza hisa za Serikali katika kampuni ya Airtel kutoka 40 hadi 49, kuongeza hisa za kampuni UDART hadi asilimia 85, kurudisha umiliki wa hisa kwa asilimia 25 katika kampuni ya MECO kutoka asilimia 2, na majadiliano yanaendelea kwa kampuni nyingine.
Bw. Mbuttuka ameongeza kutokana na maelekezo ya Mhe. Rais Magufuli, Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na ofisi yake zimenusuru mali za Serikali zilizokuwa hatarini kutoweka ambapo katika mikoa 10 iliyopitiwa, Serikali imetambua mali 531 na kufanikiwa kurejesha Serikalini majengo 337, viwanja 140, mashamba makubwa 10, maghala 41 na mali zingine 3 pamoja na kurejesha umiliki wa asilimia 100 katika kampuni ya Songwe Water Company Ltd na asilimia 40 kwa kampuni ya Liquid Storage Company Ltd.
Akizungumza baada ya kupokea gawio, Mhe. Rais Magufuli amezipongeza taasisi, mashirika ya umma na kampuni 79 zilizotoa gawio na michango kwa Serikali na ametoa siku 60 kwa taasisi, mashirika ya umma na kampuni 187 ambazo hazikutoa gawio na michango, kutoa gawio na michango hiyo vinginevyo bodi zake zitavunjwa na uteuzi wa watendaji wakuu kutenguliwa.
Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa Serikali imewekeza mitaji ya kiasi cha shilingi Trilioni 59.6 katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni 266 ikitarajiwa kuwa zitaendeshwa kwa tija badala ya kuwa tegemezi kwa Serikali ama kuendeshwa kwa hasara.
Dkt. Magufuli amesema "Kuna jumla ya mashirika, taasisi na makampuni karibu 266 lakini ukiangalia walioleta ni 79, yapo mengine 187 hayajaleta, nakuagiza Waziri wa Fedha Dkt. Philip Mpango uwatumie barua, nawapa siku 60 walete gawio au wakishindwa tuyataifishe," amesisitiza Rais Magufuli.
Vile vile, amesema ndani ya miaka mitano kuanzia 2014-15 mashirikia, taasisi na makampuni yaliyotoa gawio yalikuwa ni 24 na walikabidhi jumla ya shilingi Bilioni 130. Mwaka 2015-16 yalikuwa 25 na yalikabidhi shilingi bilion 249, mwaka 2016-17 yalipanda hadi kufikia 38 na wakatoa gawio la shilingi bilioni 677 na kwa mwaka 2017-18 yalikuwa 40 na wakakabidhi shilingi bilioni 842. Pia kwa mwaka 2018-19 mashirika, makampuni na taasisi zimepanda hadi kufikia 79 wakitoa jumla ya shilingi Trilioni 1.05.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa utendaji kazi wa taasisi hizo ni moja kati ya vyanzo muhimu vinavyopaswa kuchangia katika maendeleo ya nchini ikiwemo miradi mikubwa inayotekelezwa nchini, na amerejea kauli yake kuwa kutokana na fursa zilizopo hapa nchini zikiwemo maji, ardhi, madini, gesi, mifugo na nguvu kazi, hakuna sababu ya Watanzania kujiona masikini.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kuongezeka kwa gawio na michango kutoka taasisi hizo bado makusanyo kutoka vyanzo vya kikodi na visivyo vya kikodi hayatoshi na hivyo ametoa wito kwa taasisi hizo pamoja na wadau wengine kuongeza juhudi katika uzalishaji na ukusanyaji wa kodi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameahidi kufanyia kazi maelekezo ya Mhe. Rais Magufuli huku akibainisha kuwa kwa sasa bajeti ya Serikali inategemea mapato ya ndani kwa asilimia 70 na amesisitiza kuwa uchumi wa Tanzania utajengwa na Watanzania wenyewe.
Kesho tarehe 25 Novemba, 2019 Mhe. Rais Magufuli ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja wa maadhimisho ya kitaifa Ikulu Chamwino, ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) katika eneo la Kikombo, ataweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa jengo la Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) na ataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.