Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2018/19 na ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2018/19, Ikulu Chamwino, Mkoani Dodoma.
Katika hafla ya upokeaji wa ripoti hizo, Mhe, Rais Magufuli amempongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere kwa kazi nzuri ya ukaguzi ambayo imeonesha maeneo mbalimbali ambayo Serikali imefanya vizuri na maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi, na amewaagiza Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kufanyia kazi dosari zote zilizojitokeza katika utendaji kazi wa Serikali.
Vilevile, Mhe. Rais ameipongeza ofisi ya CAG kwa kuanza kukagua mashirika ya umma badala ya kutumia taasisi za ukaguzi za nje hatua hiyo imeokoa shilingi Bilioni 1.4, ikiwa ni pamoja na kuonesha dosari za matumizi ya fedha katika taasisi mbalimbali ikiwemo vyama vya siasa na Jeshi la Polisi.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ambaye alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu, Brig. Jen. John Mbungo kwa kazi nzuri inayofanywa na taasisi hiyo katika kudhibiti vitendo vya rushwa, kuokoa fedha na mali za umma zilizokuwa zimepotea, na pia kurejesha shilingi Bilioni 8.8 za wakulima zilizokuwa zimeibwa kupitia vyama vya ushirika vya wakulima hapa nchini.
Kutokana na kazi hiyo nzuri, Mhe. Rais Magufuli amemteua Brig. Jen. John Mbungo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kuanzia leo tarehe 26 Machi, 2020.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa kwake na viongozi wa Mikoa na Wilaya kutochukua hatua kwa wakati pale wananchi wanapodhulumiwa haki zao, na kwamba haikuwa sawa kwa wakulima kudhulumiwa shilingi Bilioni 8.8 ambazo zimesubiri timu ya TAKUKURU ya kitaifa kuchukua hatua.
Akizungumzia kuhusu maambukizi ya Virus vya Corona amesema hayawezi kuifanya serikali iache kuendelea na vikao vyake vya muhimu ikiwemo vikao vya baraza la madiwani na kutolea mfano Bunge la Jamhuri ya Muungano, na amechukua nafasi hiyo kusisitiza kuwa suala uchaguzi nalo liko pale pale.
Nae, CAG Bw. Charles Kichere amesema ripoti za ukaguzi 19 alizoziwasilisha ni za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma, miradi ya maendeleo, ukaguzi wa ufanisi, ukaguzi wa mifumo ya TEHAMA, ufuatiliaji wa mapandekezo yaliyotolewa katika ripoti za ukaguzi wa ufanisi kwa miaka iliyopita na ripoti 12 za ukaguzi wa ufanisi zinazohusu sekta mbalimbali.
Kwa upande wake Brig. Jen. Mbungo amesema utafiti uliofanywa kwa mwaka 2018/19 umeonesha kuwa idadi ya Watanzania wanaoamini kuwa vitendo vya rushwa vimepungua imeongezeka kutoka asilimia 37 (2015) hadi kufikia asilimia 71 na pia ripoti ya Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum – WEF) kwa kushirikiana na sekta binafsi imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 kwa ufanisi katika matumizi mazuri ya fedha za umma.
Rais Magufuli akipokea Ripoti ya Mwaka 2018-2019 kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) Brigedia Jenerali John Mbungo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli akizungumza na viongozi mbalimbali wa Serikali mara baada ya kupokea taarifa ya CAG na TAKUKURU.
Chanzo: globalpublishers.co.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.