SERIKALI imedhamiria kulijenga Jiji la Dodoma ili liwe la kisasa baada ya kuyapokea Makao Makuu ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Dodoma katika viunga vya stendi kuu ya mabasi inayojengwa eneo za Nzuguni jijini Dodoma leo.
Rais Dkt. Magufuli amesema “tunataka Jiji la Dodoma liwe la mfano. Miradi inayotekelezwa hapa Jiji la Dodoma ikikamilika, Jiji hili litakuwa la kisasa”. Stendi inayojengwa inatarajiwa kuunganishwa na Treni maalum. Treni hiyo itaunganisha uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Msalato na Mji wa Serikali, alisema. “Wakati wa kuijenga Dodoma umefika ikiwa ni utekelezaji wa ndoto ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere” aliongeza. Dhamira ya Serikali ni kuboresha na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa wananchi wa Dodoma.
Akiongelea miradi aliyoiwekea mawe ya msingi, Rais amesema kuwa ujenzi wa miradi hiyo unakwenda vizuri. Amesema kuwa ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa soko linalogharimu shilingi bilioni 14.649 na stendi kuu ya mabasi inayogharimu shilingi bilioni 24.033. “Shukrani Waziri Jafo kunialika kwenye shughuli hii ya maendeleo. Wana Dodoma mnapenda maendeleo". Vilevile, amewataka kutunza miundombinu inayoendelea kujengwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli amewataka wananchi wa Dodoma kujipanga na kuchangamkia fursa za Serikali kuhamia Dodoma. “Ombi langu kwa wanadodoma mjipange kufanya kazi, fursa zimepatikana. Fursa ya soko ipo. Mkichelewa wengine watakuja kuchukua fursa hizi nanyi mtabaki watazamaji“ amesisitiza Rais Dkt. Magufuli.
Akiongelea miongoni mwa sababu za kuhamishia Makao Makuu Dodoma, alisema kuwa ni kuondoa umasikini wa wana Dodoma. “Serikali imetimiza wajibu wake, suala la uchumi wa mtu mmoja mmoja ni jukumu la mtu mwenyewe. Lazima mfanye kazi” alisisitiza Rais Dkt. Magufuli.
Rais aliwapongeza wananchi wa Dodoma kwa kupata miradi mingi. ”Nawapongeza wana Dodoma, mkiongozwa na viongozi wenu, Mkuu wa Mkoa, Meya, Mkurugenzi wa Jiji kwa kupata miradi hii yote, ni miradi mingi. Pongezi pia kwa kufanya mabadiliko katika Jiji lenu. Ni Jiji hili tu lenye maendeleo mazuri…Mkurugenzi wa Jiji umenifanya niwaamini vijana kuwa wanaweza kufanya makubwa” alisisitiza.
Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli (hayupo pichani) alipokuwa akihutubia wananchi wa Dodoma kwenye Stendi Kuu ya Dodoma.
Rais Mhe. John Pombe Magufuli akiwaaga wananchi baada ya mkutano wa hadhara na wananchi wa Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.