MGANGA Mfawidhi wa kituo cha Afya Makole, Dkt. George Matiko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya Afya na kufanya maboresho kwa vituo vya Afya nchini.
Alitoa pongezi hizo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kituo cha Afya Makole mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilipofanya ziara ya kutembelea kituo hicho jana.
Dkt. Matiko alisema “tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kutupa kipaumbele kuwa miongoni mwa vituo 44 vya mwanzo kufanyiwa maboresho. Watumishi pamoja na wananchi wanafurahia kutoa na kupata huduma katika kituo hiki”.
Dkt. Matiko alisema kuwa Serikali ilitoa shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la Maabara, jengo la Mochwari, na nyumba ya mtumishi.
Kufuatia ujenzi wa majengo hayo, huduma zimeboreka. “Hata idadi ya wateja wanaokuja kupata huduma imeongezeka kutoka wastani wa wagonjwa 92,695 mwaka wa fedha 2017/2018 na kufikia wateja 256,886 mwaka 2018/2019” alisema Dkt. Matiko.
Mganga Mfawidhi huyo alisema kuwa kituo chake kilipokea vifaa vifaa tiba vyenye thamani ya 318,231,370. Alivitaja vifaa tiba hivyo kuwa ni jokofu la kuhifadhia maiti, mashine kwa ajili ya kufulia, pasi ya umeme kwa ajili ya kunyooshea mashuka, ultrasound mashine na x-ray mashine pamoja. Vifaa vingine alivitaja kuwa ni kwa ajili ya wodi ya wazazi, chumba cha upasuaji na kitengo cha maabara kwa ajili ya kuboresha huduma.
Kituo cha Afya Makole kilianzishwa mwaka 1978 hivi sasa kina watumishi 135, kikihudumia wananchi 21,407 kikiwa na vitanda 45.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.